Habari

Wakulima 8000 na Wataalam 2,303 Wanufaika na Mafunzo ya Umwagiliaji

Wakulima 8000 na Wataalam 2,303 Wanufaika na  Mafunzo ya Umwagiliaji
Aug, 16 2019

Zaidi ya wakulima 800 na wataalamu wa kilimo cha umwagiliaji wapatao 2,303 ya skimu 100 za umwagiliaji nchini wamenufaika na mafunzo ya kukuza na kuboresha kilimo cha umwagiliaji hivyo kuongeza uzalishaji zaidi.

Akizungumza wakati wa mkutano wa Tano wa Kamati ya Pamoja ya Uratibu wa Mradi wa kujenga uwezo kwa wakulima wadogowadogo Awamu ya Pili (TANCAID II) Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Marco Ndonde amesema wakulima walionufaika na mafunzo hayo wanatoka kwenye Kanda zote nane za Umwagiliaji nchni na kuongeza kuwa mafunzo hayo yameleta matokeo makubwa katika sekta ya Umwagiliaji .

“Baada ya mafunzo hayo Wakulima katika skimu mbalimbali nchini sasa wana uwezo wa kuibua miradi inayowaletea faida na kuitekeleza kwa ufanisi na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao yao” Alisema Bw. Ndonde.

Bw.Ndonde alisema mradi wa TANCAID II uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA) tangu mwaka 2015 umejikita katika kujenga uwezo wa wakulima wadogo wadogo ambao ulitekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ukiwa na lengo la kukuza na kuboresha sekta ya umwagiliaji nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa mradi wa TANCAID II Bw. Anthony Nyarubamba amesema chini ya mradi huo NIRC imetumia wataalamu wake kuandaa miongozo kabambe ya umwagiliaji (CGL) ambayo imeanza kutumika na wakulima katika maeneo mbalimbali hususan katika skimu za umwagiliaji.

Kwa kutumia miongozo kabambe ya umwagiliaji, Nyarubamba amesema wakulima sasa wanaweza kusimamia skimu zao za umwagiliaji katika ngazi mbalimbali kuanzia uibuaji wa miradi hadi usimamizi wa miundombinu inayojengwa na serikali badala ya kuiacha iharibike kama ilivyokuwa awali.

Amesema moja ya mafanikio makubwa ya Mradi wa TANCAID II ni kuwajengea uwezo maafisa kilimo, Wahandisi wa umwagiliaji wa Wilaya, Kanda na wakulima kwa ujumla katika maeneo ya uibuaji , utekelezaji, uendeshaji na matunzo ya miradi husika.

Miongozo kambambe ya umwagiliaji, Nyarubamba amesema imewajengea wakulima uwezo wa kutunza taarifa ya uibuaji, utekelezaji,uendeshaji na matunzo ya skimu zao za umwagiliaji na kupanga mapema namna ya kutunza skimu hizo kabla hazijajengwa.

Kutokana na kupewa mafunzo ya kutumia miongozo ya umwagiliaji, amesema wakulima wamekuwa na umiliki zaidi wa skimu zao, tofauti na hapo awali ambapo zilionekana kuwa haziwahusu ni mali ya serikali.

Akizungumza awali, Mhandisi Amy Mchelle amesema kutokana na kupata mafunzo wakulima sasa wanaweza kulipa asilimia tano ya mapato wanayopata baada ya uzalishaji.

Mhandisi Mchelle ameongeza kuwa miongozo kabambe ya umwagiliaji inawasaidia wakulima kupitia kamati za mradi, kusimamia ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na kuzingatia ubora unaotakiwa.

Utumiaji wa miongozo kabambe ya umwagiliaji umesaidia kupunguza migororo itokanayo na utumiaji mbaya wa maji na ardhi katika skimu mbalimbali za umwagiliaji, amesema Mhandisi Mchelle.

“Miongozo imesaidia uboreshaji na utunzaji wa miundombinu ya umwagiliaji na kuwasaidia wakulima kupanga vizuri na kutekeleza na kufuatilia nakutathimini miradi wanayoianzisha” Alisema.

Mchelle amesema utumiaji wa miongozo ya umwagiliaji imewaongezea maarifa na ujuzi wa usimamizi wa rasilimali ikiwemo maji na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbli wanayolima.

Naye Mshauri wa JICA nchini Bi. Namiko Yamada amesema kwa zaidi ya miaka 40 serikali ya Japan imetoa misaada kusaidia maendelea ya kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji.

Bi.Yamada amesema JICA chini ya mradi wa TANCAID II imeweza kusaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji na kutoa mafunzo kwa vyama vya wamwaliaji na wahandisi wa umwagiliaji.

Amesema JICA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pia imesaidia uendelezaji wa kilimo cha mpunga chini ya mradi wa TANRICE 2.