Habari

NIRC YAWAHAKIKISHIA WATANZANIA KUKAMILIKA KWA MRADI WA BBT

NIRC YAWAHAKIKISHIA WATANZANIA KUKAMILIKA KWA MRADI WA BBT
Mar, 17 2024

TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imewahakikishia Watanzania kuwa inaendelea kukamilisha ujenzi wa miundombinu, hususani katika miradi ya umwagiliaji nchini,ikiwemo mradi wa vijana wa Chinangali na Ndogowe iliyo chini ya Mpango wa Jenga Kesho Iliyobora kwa Vijana ( Building Better Tommorow (BBT); unaosimamiwa na Wizara ya KIlimo.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa, amesema katika mashamba hayo ya BBT, NIRC imehakikisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo mabwawa, visima na mashamba yanakamilika kwa wakati.

Amesema hatua hiyo imekusudia kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya kilimo na kupata matokeo chanya katika miradi hiyo ikiwemo` ajira kwa vijana na ukuaji wa Pato la Taifa kwa asiliami 10 ifikapo mwaka 2030.

“Miradi ya kilimo kwa vijana  BBT Chinangali na Ndogowe kazi inafanyika ambapo kwa upande wa Ndogowe ikiwa ni moja ya miradi ya BBT mkoani Dodoma unaogharimu zaidi ya sh. Bilioni 21.7; Tume ya Taifa ya Umwagiliaji tumehakikisha tunabadili mfumo wa umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya mabomba badala ya mifereji.

“Ukaguzi wa kazi za mkandarasi kwa kuangalia mabomba hayo yanayotoka katika kiwanda na kwenda eneo la mradi ambayo yatawekwa  kilomita 104 kuanzia bomba kubwa hadi madogo huku mkandarasi akiwa na wajibu wa kutengeneza kilomita 14 za barabarana na kilomita tano za kuingia shambani, ujenzi wa nyumba ya msimamizi wa shamba Pamoja na ujenzi wa madaraja madogo,”alisema.

Bw, Mndolwa amesisitiza kuwa mkataba wa ujenzi huo umeanza mwaka jana na kumekuwa na changamoto ya mvua hali iliyosababisha mkandarasi kusimamisha shughuli za mradi kwa muda, ambapo Tume imekuwa ikitafuta njia mbadala ya kumsaidia mkandarasi kuweza kufika eneo la ujenzi wa mradi lengo ni kuwezesha miradi hiyo ikamilike kwa wakati licha ya changamoto zinazojitokeza ikiwemo kujaa kwa maji  shambani hali inayosababisha mitambo na mashine kushindwa kufanya kazi.

Aidha Mkurugenzi Mndolwa amesisitiza kuwa Tume  inaendelea  na ukamilishaji  wa mradi wa Chinangali katika mashamba ya BBT kwa ajili ya mashamba ya vijana ambapo ujenzi wa miundombinu ikiwemo mabwawa, visima na usafishaji wa mashamba unaendelea.

“Ulazaji wa mabomba unaendelea, lengo ni kuingiza maji shambani, katika mradi huo wa Chinangali kazi zinaendelea kwa kasi ikiwemo kufungua shamba ekari 1150 ambapo tayari ekari 210 na nyinginge 56 zimeshalimwa kwa ajili ya maandalizi ya upandaji,”alisema.

Amesisitiza kuwa miradi hiyo yote inakabiliwa na mvua hali inayochangia mitambo kuzama na matumaini ya Tume kwa sasa  wakati ambapo mvua hizo  ni  kuharakasha utekelezaji wa miradi.

Aidha NIRC itahakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilika kwa wakati na kufikia lengo la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuchochea ukuaji wa uchumi.

GCU.