Habari
M/KITI BODI (NIRC) PROF, MAHOO AWATAKA WAKANDARASI KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI
MWENYEKITI wa bodi Uongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Profesa Henry Mahoo, amewataka wakandarasi wa miradi ya ujenzi miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo bwawa la umwagiliaji Membe lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma, kuhakikisha wanazingatia makubaliano ya mkataba utekelezaji wa miradi kukamilisha mradi kwa wakati.
Akizungumza jijini Dodoma katika ziara yake ya kukagua mradi huo Profesa Mahoo, amesema anaridhishwa na hatua za miradi inayosimamiwa na Tume inavyoendelea na kuwataka wakandarasi waliopewa nafasi ya ujenzi kukamilisha kwa wakati.
Amesisitiza kuwa, hatua ya Tume kutumia vifaa vyake ikiweko mitambo kukodisha kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ni hatua nzuri kwani inaongeza mapato kwa taasisi.
Amesema ujenzi wa mradi huo unaohusisha bwawa na miundombinu mingine ya umwagiliaji unaendelea vizuri.
“Mkandarasi amenithibitishia kuwa mradi utakamilika hivi karibuni na maeneo yaliyopata hitilafu yatarekebishwa ikiwemo sehemu ya ukuta katika mradi wa bwawa,” alisema.
Amesema, pia katika ziara hiyo ameridhishwa na ujenzi wa sehemu ya kutapishia maji pembezoni mwa bwawa.
“Bwawa likifikia sehemu fulani, maji yanatakiwa yatoke ili bwawa lipumue na lisiharibike ujenzi wa sehemu hiyo imefikia hatua nzuri,”alisema.
Kwa upande wake Mhandisi Umwagiliaji mkoa wa Dodoma ambaye ni Meneja wa mradi huo kutoka NIRC Mhandisi Osward Urasa amesema mradi huo umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Agosti mwishoni na kufikia lengo la wakulima wa eneo hilo kuwa na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji.
GCU.