Habari
WAZIRI MKUU MHE, KASSIM MAJALIWA AIAGIZA (NIRC) KUSIMAMIA MIRADI YA UMWAGILIAJI KWA WELEDI.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewaelekeza watendaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji makao makuu, mikoa, wilaya pamoja na wasimamizi wa miradi ya Umwagiliaji inayoendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali nchini kusimamia ujenzi wa miradi hiyo kwa weledi na uaminifu mkubwa ili thamani ya fedha zinazotolewa na serikali zitumike kuwanufaisha wakulima ambao ndio walengwa wa miradi hiyo.
Mhe, Majaliwa ameyasema hayo mara baada ya kushuhudia utiliaji Saini wa mikataba 20 ya ujenzi, ukarabati, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wakandarasi 11 walioshinda Zabuni.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imeongeza bajeti ya umwagiliaji kutoka Tsh, Bilioni 41 mwaka 2021 kufikia Bilioni 365 Mwaka 2023 – 2024, dhamira ya Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuongeza fedha za utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji kila mwaka kwakuwa mchango wa sekta ya Umwagiliaji ni muhimu katika kuinua Uchumi wa mkulima mmoja mmoja, kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na malighafi kwaajili ya viwanda nchini.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amewahasa Wabunge katika Majimbo yenye miradi ya umwagiliaji kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi na kuhimiza Halmashauri nchini kutenga ardhi kwaajili ya shughuli za umwagiliaji.
Kwaupande wake Waziri wa Kilimo Mhe,Hussein Bashe amesema mbali na kuwatumia wakandarasi katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2023 – 2024 inakwenda kutekeleza miradi minne ya umwagiliaji kupitia mfumo wa Force account, kwa kutumia wataalam wa ndani. Aidha Mhe, Bashe ameendelea kusema kuwa miongoni mwa mikataba 20 iliyosainiwa jumla ya kampuni 11 za ndani zimepatiwa kandarasi za ujenzi wa miradi hiyo kwa lengo wa kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani.
Naye Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa amesema miradi mingi ya Umwagiliaji inatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, hivyo kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa skimu zinazoendelea kujengwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023 – 2023/2024 kutaongeza eneo la Umwagiliaji kufikia Hekta 983,465.46 sawa na asilimia 81.9 na kufanya eneo la Umwagiliaji kufikia Hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025 ambapo pia kutaongeza ajira 1,352,127.
Aidha Bw, Mndolwa amesemaTume ya Taifa ya Umwagiliaji imefanikiwa kununua vitendea kazi kwa ajili ya watumishi wa Tume ikiwemo magari (48), mitambo 15 na magari makubwa (heavy trucks) 17 kwa ajili ya usimamizi, ufuatiliaji na ujenzi wa miradi ya umwagiliaji. Aidha, Tume imefungua ofisi 121 za Wilaya za Umwagiliaji na kuajiri Watumishi 320 kwa ajili ya kusimamia miradi ya umwagiliaji katika ngazi ya Mikoa na Wilaya.