Habari
BODI YA UONGOZI NIRC YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI SKIMU YA MKOMBOZI
Bodi ya uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, imewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi skimu ya Mkombozi,kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo, ili kuendana na muda wa mkataba. Lengo ni kuwa mradi huo uwe na tija kwa wakulima baada ya kukamilika kwake na ili pia sekta ya umwagiliaji kufikia malengo ya agenda 1030.Hayo yamejiri katika ziara ya Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na menejimenti ya Tume, katika mradi wa ujenzi wa skimu hiyo iliyopo katika kata ya Mboliboli na kata ya Itunundu katika tarafa ya Pawaga,halmashauri ya wilaya ya Iringa vijijini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya uongozi ya Tume, Prof. Henry Mahoo, amesema bodi hiyo imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, na kuwaagiza wakandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi, ili kuwanufaisha wakulima wa mkoa wa Iringa, na kuwa na uhakika wa chakula nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa, amesema thamani ya mradi huo wa Umwagiliaji ni zaidi ya shilingi bilioni 52,ambapo mradio huo unatadajiwa kukamilika February 2024, ambapo una jumla ya hekta 6000.
Ameongeza kuwa, matarajio ya mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa mpunga na kuwawezesha wakulima kulima zaidi ya mara moja, kwa mwaka.
Baadhi ya wakazi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo,ikiwemo kata ya Pawaga,wameipongeza serikali kwa kuwekeza fedha nyingi kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
Kukamilika kwa ujenzi wa skimu za Mkombozi Lot 1, Lot 2, 3 na 4, kutaongeza eneo lenye miundombinu ya umwagiliaji,kufikia ekari 15,000.
Pia eneo linalomwagiliwa kuongezeka kutoka ekari 4,500 zinazomwagiliwa kwa njia za asili kwa sasa, hadi kufikia ekari 15,000 zenye miundombinu bora ya umwagiliaji.
Aidha, kukamilika kwa mradi huu na matumizi bora ya kanuni za kilimo, kutaongeza uzalishaji,ambapo uzalishaji wa zao la mpunga unategemewa kuongezeka kutoka tani 2 kwa hekta hadi kufikia tani 5 kwa hekta.
Hata hivyo,lengo kuu la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ni kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika, kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,kwa kuzingatia matumizi bora ya maji ili kuongeza uzalishaji wa mazao kwa tija, kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.