Habari

MKURUGENZI MNDOLWA AWAASA WAKULIMA MVOMERO KUTUNZA VYANZO VYA MAJI.

MKURUGENZI MNDOLWA AWAASA WAKULIMA MVOMERO KUTUNZA VYANZO VYA MAJI.
Jun, 10 2022

Kulia Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa, akionesha sehemu ya daraja la mto Mvomero, halipo katika picha. Lililoharibiwa vibaya na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabia nchi pamoja na shughuli za kibinadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa, amewaasa wakulima nchini kutunza vyanzo vya maji. Kwa kutokufanya shughuli za kibinadamu hususani za kilimo ndani ya mita sitini (60), ili kunusuru kuharibika kwa kingo za mito kunakopelekea uharibifu wa Miundombinu ya kilimo cha Umwagiliaji.

Bw. Mndolwa ameyasema hayo mapema alipokuwa akizungumza na wakulima wa skimu ya Umwagiliaji Msufini iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro. Inayotumia maji kutoka mto Mvomero kama chanzo cha maji ya kilimo cha Umwagiliaji. Ambapo ameshuhudia uharibifu mkubwa uliofanyika kutokana na shughuli za kilimo zisizo rasmi.

Aliwashauri viongozi wa Serikali ya kijiji kushirikiana kulinda vyanzo hivyo vya maji kwa manufaa ya kila mwananchi na aliendelea kusema. “Hatulindi vyanzo vya maji ya kunywa tu, hata vya kilimo na kuzuia uharibifu unaofanywa na binadamu wenzetu, asili inaharibiwa na binadamu.”Alisisitiza

Bw. Mndolwa aliagiza wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wataalam kutoka Halmashauri, kufanya mapitio ya mto na chanzo nakuona athari iliyotokana na mafuriko yaliyopita katika mto huu. 

Katika zoezi hilo wataalam watatakiwa kuja na mapendekezo yanini kifanyike ili kurekebisha athari za mafuriko, hali itakayopelekea skimu ya Msufini kuanza kufanya kazi.