Habari

MABORESHO YA MIUNDOMBINU YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MBARALI YAWANUFAISHA WAKULIMA

MABORESHO YA MIUNDOMBINU YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MBARALI YAWANUFAISHA WAKULIMA
Oct, 22 2018

Imeelezwa kuwa maboresho ya miundo mbinu ya skimu ya kilimo cha umwagiliaji ya Igomelo iliyopo wilayani Mbarali Mkoani Mbeya, imewanufaisha kwa namna mbalimbali wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha mbogamboga.

Hayo yameelezwa jana na Mhandisi wa kanda ya Mbeya wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Elibariki Mwendo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea skimu hiyo.

Mhandisi Mwendo alisema kuwa, Serikali imetumia kiasi cha shilingi Milioni mia mbili hamsini (250Milioni) kukarabati miundo mbinu ya skimu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa banio kubwa linalotoa maji katika chanzo cha maji cha mto Mbarali na mifereji inayopeleka maji mashambani.

“katika skimu hii wakulima wanajikita zaidi katika kilimo cha mbogamboga kama vile vitunguu, nyanya, matango, na hata zao la mpunga, ambapo kabla ya marekebisho na maboresho ya miundo mbinu hii, hali haikuwa nzuri kwani wakulima walikuwa wanajichotea maji kiholela ilikuweza kumwagilia mazao yao, lakini kwa sasa kama mnavyoona, maji yana kwenda moja kwa moja mashambani kwa utaratibu maalumu livyopangwa ambapo kila mkulima ana zamu yake ya kuingiza maji mashambani tayari kwa kilimo, jambo ambalo limepelekea wakulima hawa kuongeza uzalishaji katika mazao wanayolima nakujiongeza pato la familia.” Alisisitiza Mhandisi Mwendo.

Mmoja wa wakulima wanaojishughulisha na zao la kilimo cha vitunguu katika skimu hiyo Bw. Yohana Mbuna (52) amesema amekuwa akijishughulisha na kilimo katika skimu hiyo kwa takribani miaka ishirini sasa, “Kabla ya maboresho katika skimu hii hali ilikuwa mbaya kwanza tulikuwa tunalima bila kufuata utaratibu, tulikuwa tunagombania maji na hata mavuno hayakuwa mengi kwa heka moja nilikuwa napata magunia 30 lakini kwasasa kwa heka moja ninaweza kupata zaidi ya magunia 100 na hii hunisaidia kupata fedha za kusomesa watoto wangu, na ninalima vitunguu kama zao la biashara, pamoja na hilo mazao mengine ya chakula kama mpunga ninalima kwa ajiliya familia yangu.” Alisema Bw. Mbuna.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Umwagiliaji kanda ya Mbeya Mnadi Taribo amesema kupitia Mradi wa kuwajengea Uwezo wataalam na wakulima Tanzania Capacity Building for Irrigation Development (TANCAID) wakulima wameweza kupata Elimu kuhusu mafunzo matumizi sahihi ya maji katika kilimo hususan kilimo cha mpunga kitaalam kilimo shadidi, usimamizi bora wa maji na kanuni sahihi za kilimo.


Aliongeza kwa kusema kuwa sambamba na hilo, kupitia mradi uliopita miaka miwili nyuma wa (PHRD) Policy Human Resource Development uliofadhiliwa na Bank ya Dunia, pamoja na wakulima kupatiwa mafunzo pia walipata vifaa vya kuvunia mazao kama vile Mpunga, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao yao na mashine za kukobolea zao la mpunga, jambo ambalo limesaidia pia vijana wengi kupata ajira na wakulima kujua matumizi sahihi ya maji, kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza thamani ya mazao.

Akiongelea changamoto ya wadudu aina ya onion thrips wanaoshambulia zao la vitunguu na kusababisha mnyauko, Bw. Taribo amesema kuwa serikali imeshafanya jitihada ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuchukua sampuli za wadudu hao na kupeleka katika chuo cha Kilimo Uyole kwa ajili ya kufanyia tafiti.

Awali imeelezwa kuwa kanda ya kilimo ya mbeya inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Songwe ina jumla ya ukubwa wa Hekta laki 268,350 ambapo Hekta 66,974 zimeendelezwa na Hekta 201,376 hazijaendelezwa na zipo kwenye mpango kabambe wa kitaifa wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji unaolenga kuendeleza hekta milioni moja (1,000,000,) katika awamu ya kwanza ya 2020 mpaka 2025 na awamu ya pili ya 2025 - 2035.