Habari

Wakandarasi watakiwa kuzingatia viwango vya ujenzi wa miundo mbinu ya umwagiliaji

Wakandarasi watakiwa kuzingatia viwango vya ujenzi wa miundo mbinu ya umwagiliaji
Oct, 23 2018

WAKANDARASI wanaojenga miundo mbinu ya umwagiliaji nchini wametakiwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika kufanya kazi hiyo.

Wito huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Usanifu na Uratibu wa Sekta Binafsi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Muyenjwa Maugo katika semina ya mafunzo ya siku tatu yanayofanyika katika Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora kwaajili ya kuwajengea uwezo wahandisi na wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji nchini.

Maugo amesema mkandarasi yeyote ambaye hata zingatia ubora na viwango vinavyotakiwa atasimamishwa na kuondolewa kabisa na kutopewa kazi tena ya kujenga miundo mbinu ya umwagiliaji nchni.

Aidha Maugo amewataka wahandisi wa Kanda wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji nchini ili kuhakikisha kuwa serikali inapata dhamani halisi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa husika huo.

Amesema washiriki wa mafunzo hayo wapatao sitini wanatoka katika kanda nane za umwagiliaji, wahandisi 17 kutoka Halmashauri 17 za wilaya na wakandarasi 11 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.

Maugo amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwakushirikiana na serikali ya Japan inatekeleza mradi wa miaka minne wakujenga uwezo kwa wataalam ili kukuza maenedeleo ya skimu za umwagiliaji chini ya mipango ya kilimo ya wilaya Awamu ya II (TANCAID II) .

Kwa mujibu wa Mhandisi Maugo kupitia mradi huo ulioanza mwaka 2015 serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Japan imepanga kufufua skimu za umwagiliaji hivyo mhandisi umwagiliaji ama mkandarasi atakayebainika kushindwa kutekeleza mradi chini ya kiwango sheria itachukua mkondo wake

Kwa upande wake Mshauri Mkuu wa Mradi kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) Yoichi Yamauchi amesema mradi huu unalenga kuwasaidia wataalamu katika ngazi ya wilaya kuibua, kuanzisha , kutekeleza na kutunza miundo mbinu na skimu za umwagiliaji nchini.

Yamauchi amesema kuwa chini ya mradi wa TANCAID II vyama vya wamwagiliaji nchini vimeweza kupata mafunzo kuhusu kupanga na kusimamia skimu za umwagiliaji kwa mujibu wa miongozo ya umwagiliaji ambayo serikali imeweka.