Habari

‘SITASITA KUSITISHA MKATABA WA MKANDARASI YOYOTE YULE KAMA HATAKUWA NA VIGEZO VINAVYOTAKIWA’ – MNDOLWA

‘SITASITA KUSITISHA MKATABA WA MKANDARASI YOYOTE YULE KAMA HATAKUWA NA VIGEZO VINAVYOTAKIWA’ – MNDOLWA
Jun, 11 2022

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, amesema hatasita kusitisha mkataba wa mkandarasi yeyote yule atakayekosa vigezo vinavyotakiwa. Hata kama atakuwa ameanza kazi ya ujenzi ama ukarabati wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.

Bw. Mndolwa amesema hayo mapema jana (Jumamosi, Juni 10, 2022), alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro. Baada ya ziara ya ukaguzi maalum wa skimu ya kilimo cha umwagiliaji Msufini. Ambapo yalijitokeza makosa ya kitaalam kabla ya ukarabati wa skimu hiyo yaliyopelelekea miundombinu ya skimu hiyo kutofaa.

“Niliamua kuitembelea skimu ya Msufini, wilayani mvomero kwa sababu ilikuwa na matatizo. Ni skimu ambayo tayari alikuwa amepewa mkandarasi kwa ajili ya kuiendeleza, lakini maandalizi ya skimu ile hayakuwa mazuri. Kiasi cha kupelekea wataalam kuruhusu mkandarasi kwenda site wakati hakukuwa na site ambayo inaweza kutekeleza kazi hiyo.” Alisisitiza Mndolwa

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa

Picha ikimuonesha Bw. Raymond Mndolwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mwenye shati la Draft akizungumza na wataalam alipokuwa kwenye banio la skimu ya kilimo cha umwagilijai Dakawa Wilayani Mvomero.

Aliendelea kufafanua kuwa mapungufu haya yapo ndani ya Ofisi yake. “Nimewaambia hakuna mradi ambao tutaufanya bila kuwa na uhakika na chanzo cha maji. Skimu hiyo imefanyiwa   kazi wakati chanzo cha maji tayari kilikuwa kimekwisha athirika.” Alibainisha Mkurugenzi Mndolwa

Aidha Bw. Mndolwa ametoa maelekezo kwamba Mradi wa kilimo cha Umwagilijai Msufini hauwezi kutekelezeka, hivyo wataalam warudi wakaanze kujipanga upya kufanya tafiti.

Akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Bw. Mndolwa aliomba ushirikiano na Uongozi wa Wilaya hiyo katika suala zima la elimu kwa umma. Kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji kwamba jambo hilo lipewe kipaumbele.

Na kushauri kuwe na ushirikiano na wadau kama vile, TANROADS ambao walitengeneza barabara inayoelekea Turiani. Yenye Daraja ambalo limesetiwa na kuhamisha mto Mvomero kiasi kwamba kwa baadae inaweza kuleta athari kwenye makazi ya watu.

Mkurugenzi Mndolwa alibainisha kwamba, “Wengine wote wahakikishe kama wanasema wanafanya miradi yoyote wawe na taarifa zote. Uzembe kama uliotokea Msufini ni uzembe wa wataalam ndani ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Hakuna vinginevyo na wao watawajibika kwa namna yao na mimi sitakubali uzembe kama huo uliotokea ujirudie tena.”

Mndolwa aliendelea kusema kwamba, hatutafanya mradi ambao hakuna wataalam. “Kwa hiyo tutahakikisha kwanza wataalam wanapita, tutahakikisha tunawashirikisha na wale wengine (wadau). Kama watu wa Bonde, watu wa mazingira na kuhakikisha kwamba, mradi unaotakiwa kujengwa unakuwa endelevu. Kwa hiyo hata kama tunataka kujenga bwawa lazima tufikirie, hili bwawa au skimu je, miundombinu hii itakuwa endelevu kwa muda gani? Kwa hiyo kitu muhimu nitachotaka kusema ni kwamba utaalam nitautumia kwenye kazi yangu kuhakikisha kwamba unatupa majibu sahihi.” Alisisitiza

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Bi. Halima Okashi, alisema kuwa kumekuwa na ukakasi katika ukarabati wa Skimu ya kilimo cha Umwagiliaji Msufini. Na changamoto ni kubwa katika skimu nyingi wilayani Mvomero, na fedha nyingi za Serikali zimetumika na kushauri kuwepo kwa ushirikishwaji mkamilifu wa wadau katika kazi hizo.