Habari

Mafunzo maalum kwa Wahandisi

Mafunzo maalum kwa Wahandisi
Jun, 28 2018

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetoa Mafunzo maalum kwa wahandisiwatakaosimamia ujenziwa miundombinu ya umwagiliaji kwenye skimu kumi na sita(16) zitakazojengwa mwaka ujao wa fedha, 2018/2019 kutoka kwenye kanda nane (8) za Tume ya Taifa ya umwagiliaji, Halmashauri za wilaya pamoja na wakandarasi, ikiwa na lengo lakuwajengea uwezo uelewa na uzoefu zaidi wahandisi hao katika usimamizi wa mikataba na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Akizungumza katika warsha hiyo ya mafunzo ya siku tatu iliyofanyika Mkoani Shinyanga, Kaimu Mkurugenzi wa uendelezaji wa miundombinu ya Umwagiliaji kutoka Tume hiyo Mhandisi, Pascal Shayo, alisema kuwa Tume imetoa Mwongozo wa ujenzi wa skimu za umwagiliaji na alisisitiza ya kuwa, wahandisi waliopewa mafunzo hayo wanatakiwa wasimamie ujenzi wa skimu hizo kwa kufuata mafunzo waliyoyapata ili kuhakikisha miundombinu hiyo inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa.

“Mhandisi atakayeshindwa kusimamia vizuri atachukuliwa hatua kwani kwa kupitia mafunzo haya wameshapata uelewa wa kutosha.”Alisisitiza

Kwa Upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Sanifu na Uratibu wa Sekta Binafsi kutoka katika Tume hiyo Mhandisi Muyenjwa Maugo alisema warsha hiyo ina lengo la kuhakikisha miradi yote ya umwagiliaji inajengwakatika kiwango elekezi na wananchi wanapata huduma iliyokusudiwa katika kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha mazao bora.

“Lengo kubwa ni kujenga uwezo kwa wahandisi na wataalam wa umwagiliji ili kuweza kusimamia miradi ya umwagiliaji kwa ufanisi, na kupitia miradi hii tunaweza kuwafundisha wahandisi namna ya kutumia mwongozo uliyopo katika kusimamia shughuli za umwagiliaji.” Alibainisha Maugo.

Awali imeelezwa kuwa ,ujenzi wa skimu hizo kumi na sita (16) utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.5 ambazo ni mkopo kutoka serikali ya Japani kupitia shirika lake la maendeleo la kimataifa (JICA).