Habari

Mambwana Shamba Wahimizwa Kutumia Tafiti Katika Uzalishaji

Mambwana Shamba Wahimizwa Kutumia Tafiti Katika Uzalishaji
Aug, 14 2018

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Nchini imesema kuwa ili mkulima aweze kufanikiwa katika uzalishaji wenye tija na kukuza pato la Taifa ni lazima mabwana shamba wa Wilaya, Kata na Kijiji kutumia tafiti zilizofanywa na Tume hiyo.

Wito huo ulitolewa jana na Kaimu mtafiti, idara ya utafiti wa teknolojia za umwagiliaji Mhandisi Ammy Mchelle, wakati wa mahojiano yake na waandishi wa habari waliotembelea katika banda lao la maonesho ya nane nane yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi Mjini Bariadi.

Kaimu huyo alisema kuwa Tume ya Umwagiliaji imefanya tafiti katika miradi mbalimbali ya umwagiliaji ili kusaidia kutatua na kupata ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza katika shughuli za umwagiliaji kwa wakulima.

Alisema ni vyema sasa tafiti hizo zikatumika ipasavyo na mabwana shamba kwa kushirikiliana na wakulima ili kujua kiundani namna miundombinu ya umwagiliaji inavyoweza kutumika kwa usahihi.

“kupitia tafiti zetu tunazozifanya katika sekta ya umwagiliaji zitasaidia kutambua mambo muhimu ambayo yanaweza kuzaa matunda katika ukuaji wa kilimo cha umwagiliaji naamini tafiti zikitumika vema zitasaidia pia kutoa mwongoza wa matumizi sahihi na yanayofaa katika kuzalisha”alisema Mchelle

Nae Kaimu Mkurugenzi wa idara na uhamasishaji wa teknolojia za umwagiliaji Dr. Eliakimu Chitutu alitaja baadhi ya miradi wanayoifanyia tafiti kuwa ni utafiti juu ya miundombinu ya umwagiliaji na matumizi sahihi ya miundombinu katika uzalishaji.

Dr. Chitutu alisema Tume hapo awali walikuwa haijajikita kufanya tafiti lakini kwa sasa inafanya na alisisitiza taasisi binasfi, maafisa ugani na watu binafsi ni vyema wakazitumia tafiti hizo kama kweli wanataka kufanya mabadiliko katika sekta ya umwagiliaji .

Juma Hussein mkulima wa mbogamboga mjini Bariadi alisema kuwa, endapo wataalamu wa kilimo katika maeneo yao watatumia vyema tafiti za Tume ya Umwagiliaji wakulima wataweza kubaini namna gani ya kutatua changamoto za umwagiliaji wakati wa kilimo .