Habari

MAZAO YA MBOGAMBOGA YACHANGIA KASI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

MAZAO YA MBOGAMBOGA YACHANGIA KASI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI
May, 05 2020

IMEELEZWA KUWA, uhitaji mkubwa wa mazao ya mbogamboga katika Jiji la Mbeya na mikoa ya Jirani umechangia kwa kiasi kikubwa kasi ya kilimo cha Umwagiliaji katika skimu ya kilimo hicho ya Bonde la Uyole iliyopo Jijini Mbeya.

Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa Umwagiliaji katika Bonde hilo Bw. John Soda, alipokuwa kizungumza na wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambapo amesema kuwa kutokana na uhitaji huo kuwa juu vijana wengi wamejikita katika shughuli hizo za kilimo rafiki na rahisi kisichotegemea mvua katika skimu hiyo yenye ukubwa wa eneo zaidi ya hekta mia moja (100).



Bwana Soda amesema kuwa, pamoja na mahitaji ya aina hiyo ya mazao kuwa juu kilimo hicho pia kimewasaidia wakulima kujipatia ajira inayowapelekea kujiongezea kipato binafsi, kupeleka watoto wao shule na kubadilisha hali ya maisha yao kwa ujumla.

Awali akiongea katika skimu hiyo ya kilimo cha umwagiliaji Bw. Soda aliishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji hususan mfereji wenye urefu wa mita elfu nne na mia tano (4,500) na kuiomba serikali kumalizia kusakafia kipande cha mita elfu moja na mia tano (1,500) zilizobakia katika eneo hilo la umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji.

Sambamba na hilo Bw. Soda aliiomba Serikali pia kusaidia katika upatikanaji wa soko la uhakika ambalo litapelekea mkulima kumfikia mnunuzi moja kwa moja bila kupitia dalali.

“Pamoja na hilo Tunaiomba pia Serikali kutusaidia kupata teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji inayotumia maji kidogo kama vile kilimo cha Drip Irrigation” Alisisitiza Bw. Soda.