Habari

UJENZI WA MIRADI 21 YA UMWAGILIAJI SASA RASMI, MNDOLWA AAHIDI KUSIMAMIA KWA WELEDI.

UJENZI WA MIRADI 21 YA UMWAGILIAJI SASA RASMI, MNDOLWA AAHIDI KUSIMAMIA KWA WELEDI.
Aug, 10 2022

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa amesema Taasisi yake imeanza rasmi jukumu la kusimamia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022 – 2023  ya Shilingi Bilioni 361.5 na nyongeza ya shilingi Bilioni 71 kutoka kwa wafadhili na mikopo midogo hivyo kuitimisha jumla ya shilingi Bilioni 432 zitakazotumika kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji nchini ikiwemo skimu 21 na mabwawa 14 ya umwagiliaji katika baadhi ya skimu zitakazojengwa chini ya Wizara ya Kilimo.

Akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari kwa nyakati tofauti  katika viwanja vya Nane nane (John Mwakangale) jijini Mbeya mara baada ya kutiliana saini mikataba ya makubaliano ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na kampuni 17, Bw, Mndolwa amesema jukumu la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ni kutekeleza ujenzi wa zaidi ya hekta 95 elfu za umwagiliaji na kwa mujibu wa maagizo ya serikali pamoja na ilani ya chama tawala kuhakikisha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 1,200,000 mwaka 2025.

Hivyo tume inajukumu la kujenga miundombinu hiyo kwaniaba ya serikali na kuwaelimisha wakulima mbinu bora za kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuwapa wakandarasi maeneo ya kujenga skimu na mabwawa pamoja na kuwasimamia ili wajenge miradi hiyo kwa ufanisi unaotakiwa.

“Ni wahakikishie watanzania kuwa tutatekeleza miradi hiyo kwa ufanisi  na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakuwa  endelevu.”

Bw, Mndolwa ameongeza kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuja na mpango wa (Block farming) wenye lengo la kufungua mashamba makubwa na kuwapa vijana walime kwa lengo la kuwawezesha vijana kujiajiri katika shughuli za kilimo biashara, hivyo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaandaa mashamba hayo mkoani Dodoma na utafuatiwa na mkoa wa Mbeya na kisha mikoa mingine nchini.

“Mheshimiwa rais Samia Suluhu Hassan anataka kuwaona vijana, nguvu kazi ya taifa hili iende kwenye uzalishaji isiende kwenye kuuza vitu vidogo vidogo, kijana anaweza kuwa na Bodaboda na akatumia bodoboda yake kwa shughuli za shamba na abiria katika muda wa ziada.”

Kwakufanya hivyo nchi itakuwa na chakula cha kutosha na vijana watakuwa na ajira, hivyo kuitimisha agenda 10/30 ya kilimo ni biashara.

Bw, Mdolwa ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya umwagiliaji pamoja na watendaji wakuu Wizara ya Kilimo kwa kumuunga mkono hivyo kurahisha utendaji wake.

GCU – NIRC.