Habari

Mpango kabambe wa kilimo cha umwagiliaji

Mpango kabambe wa kilimo cha umwagiliaji
Jul, 27 2018

Serikali imefanya mapitio ya mpango kabambe wa Taifa wa umwagiliaji wa mwaka 2002 kupitia Tume ya Taifa ya umwagiliaji ikiwa na lengo la kuongeza uzalishaji kwa hekta zaidi ya milioni moja nchini kufikia mwaka 2025 kupitia kilimo cha umwagiliaji ili kuweza kukuza uchumi, kuongeza chakula na malighafi za viwandani.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Usanifu na Sekta Binafsi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Muyenjwa Maugo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Bw. Maugo Alisema kuwa, Mpango huo kabambe unabanisha kuwa kupitia kilimo cha umwagiliaji chenye kutumia maji ya uhakika na kwa wakati mkulima anaweza kuzalisha awamu mbili au tatu kwa mwaka, na kuwa na uhakika wa chakula kwa kuzalisha tani nane (6) mpaka kumi (10) kwa Hekta tofauti na kilimo cha kutegemea mvua za msimu ambapo mkulima anaweza kupata tani mbili (2) za mazao kwa mwaka kwa hekta, hivyo kwa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji malighafi za viwandani zinaweza kupatikana kwa wakati na kufikia hazima ya serikali ya kuijenga Tanzania ya viwanda.

“Mpaka sasa eneo la hekta laki 475 ndilo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji nchini ambayo ni sawa na 1.6% kati ya hekta milioni 29.4, na kuchangia asilimia 24 (24%) ya uzalishaji wa chakula nchini, tuna uwezo wa kuongeza na kufikia asilimia 50 (50%) na tuna lengo la kufikia Hekta milioni moja” Alisisitiza Maugo.

Aliendelea kusema kuwa Mpaka sasa kuna skimu 2947 za kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo skimu zinazofanya kazi ni 1976, na mpango kabambe upo na malengo ya kuzifufua skimu zisizofanya kazi ili ziweze kufanya kazi.

Awali Mhandisi Maugo alisema kuwa mapitio ya Mpango huo kabambe wa kilimo cha umwagilaji unafanyika kwa ushirikiano wa Shirika la Maendeleo la Japan JICA.