Habari

Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili Kuelekea Tanzania ya Viwanda

Mpango  Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili Kuelekea Tanzania ya Viwanda
Aug, 14 2018

Kuelekea Tanzania ya viwanda katika eneo la kilimo cha umwagiliaji, Mpango kabambe wa maendeleo ya kilimo awamu ya pili una lengo la kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua kwa kuongeza eneo la umwagiliaji nchini, kutoka hekta 461,326 mwaka 2014 hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2025.

Hayo yameelezwa leo wakati wa maonyesho ya wakulima nanenane katika viwanja vya Nyakabindi , Mjini Bariadi na Mhandisi Ebenezer Kombe kutoka kanda ya Umwagiliaji ya Mwanza alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.

Mhandisi Kombe amesema kuwa ili kufanikisha hayo, serikali itashirikiana na sekta Binafsi kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga mifereji mikuu, mifereji ya kati na mabwawa ya kuhifadhia maji kwenye maeneo yenye ukame.

Aidha Bw. Kombe alisema , Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri husika itahamasisha wakulima kupitia vyama vya umwagiliaji kuchangia katika ujenzi wa mifereji midogo ya kuingiza maji mashambani na kushiriki katika kuitunza mifereji hiyo.

“Tutawafundisha wakulima kuzalisha kwa tija na ufanisi kwa kutumia miundombinu iliyopo ikiwa ni pamoja na kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka, kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa mfano kilimo shadidi cha mpunga ( kilimo chenye matumizi kidogo ya maji ).” Alisisitiza.

Sambamba na hilo, mhandisi Kombe aliongeza kusema kuwa,serikali inatilia mkazo kukamilisha skimu zote za umwagiliaji ambazo zilijengwa miaka ya nyuma jambo ambalo litasaidia wakulima wadogo na wa kati kuongeza uzalishaji wa chakula cha kutosha na ziada kwa ajili kuongeza kipato cha mkulima na Taifa kwa ujumla.

Alisema lengo lingine kubwa ni kujenga mabwawa ya uvunaji wa maji yamvua na kuhamasisha matumizi ya maji chini ya ardhi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuweza kuhimili na kukabiliana na athari na hasara zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Afisa Kilimo toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Petro Sarwat alisema Kupitia mwongozo kabambe wa kuendeleza kilimo chaumwagiliaji, wakulima wanatakiwa kufuata taratibu zilizoelekekezwa ikiwa ni pamojana hatua za kufuata katikakuibua miradi ya umwagiliaji, kuitekeleza, kuindesha na kuitunza.

“Hukonyuma miradi ya umwagiliaji ilikuwa ikikosa utaratibu mzuri wa uendeshaji na matunzo, jambo lililopelekea miundombinu kutokufanya kazi kwa ufanisi nakuharibika kwa muda mfupi baada ya ujenzi kukamilika, hivyo basi Serikali inafanya jitihada za kutoa elimu sahihi kuhusu mwongozo ili kuifanya miundombinu kuwa endelevu.” Alibainisha

Awali imeelezwa kuwa kilimo cha umwagiliaji huleta uhakika wa chakula na hatimaye kusaidia mali ghafi zitakazoweza kutumika katika viwanda na kufikia azima ya serikali ya awamu ya Tano ya kuijenga Tanzania ya viwanda.