Habari

WAHANDISI KILIMO CHA UMWAGILIAJI WATAKIWA KUSIMAMIA UJENZI NA UKARABATI WA MIUNDOMBINU KWA UMAKINI

WAHANDISI KILIMO CHA UMWAGILIAJI WATAKIWA KUSIMAMIA UJENZI NA UKARABATI WA MIUNDOMBINU KWA UMAKINI
Jun, 06 2022

NZEGA - TABORA

Wahandisi wa Kilimo cha Umwagiliaji nchini wametakiwa kusimamia kazi za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo ya miradi kwa umakini na ueledi mkubwa kwani, kazi hizo zinatakiwa kufanyika  kwa wakati kulingana na mkataba kwa wakandarasi  na hakutakuwa na muda wa nyongeza kwa mkandarasi ambaye atafanya kazi kwa kuchelewa na chini ya kiwango.

Ukarabati Idudumo Picha na. 2

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki, na Kaimu Mkureugenzi wa Idara ya Miundombinu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Ntonda Kimasa, alipokuwa katika skimu ya Kilimo cha Umwagiliaji Idudumo wilayani Nzega Mkoani Tabora.

Mhandisi Kimasa alisema, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi milioni 700 fedha za ndani, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao una bwawa na utahusisha  kuboresha mfereji mkubwa wenye urefu wa kilimita mbili pamoja na mifereji mingine mitano ya upili ya kupeleka maji mashambani.

Baada ya kufanya ukaguzi wa ujenzi na ukarabati katika skimu hiyo Mhandisi Kimasa alisema “Kwa ujumla kazi inaendelea vizuri na ninaamini kazi itakamilika na mkandarasi ataikabidhi kwa wakati.” Alisisitiza.

Akiongea kwa niaba ya wakulima wa chama cha umwagiliaji Idudumo, Bwana Stefano Honoli ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya ujenzi, amemshukuru Mbunge wa Nzega Mhe. Hussein Bashe ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, kwa jitihada anazofanya katika kuboresha sekta ya kilimo cha umwagiliaji na kuiomba serikali ya awamu ya sita kuendelea na awamu nyingine ya ukarabati katika skimu hiyo kwa kutoa mafungu zaidi ya fedha, kwani skimu hiyo inauwezo wa kulisha mkoa mzima wa Tabora.

Kazi ya ukarabati wa skimu ya kilimo cha umwagiliaji Idudumo inayofanywa na mkandarasi mzalendo M/S Explicit Main Constractors Ltd. inategemewa kukamilika mwezi wa kumi mwaka huu, na utasaidia wakulima kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika kipindi chote cha mwaka.