Habari

TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KUJENGA MABWAWA 14 NA HEKTA ELFU 10 ZA UMWAGILIAJI KWA AJILI YA UZALISHAJI WA MBEGU, SHILLINGI BILIONI 420 KUTUMIKA.

TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KUJENGA MABWAWA 14 NA HEKTA ELFU 10 ZA UMWAGILIAJI KWA AJILI YA UZALISHAJI WA MBEGU, SHILLINGI BILIONI 420 KUTUMIKA.
Jun, 16 2022

Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe, amesema kwa Mwaka wa fedha ujao Wizara yake itatumia Shilingi Bilioni 420, katika ujenzi wa Miundombinu ya Skimu za umwagiliaji. Ikiwemo Hekta elfu kumi kwa ajili ya uzalishaji wa Mbegu, ambapo wadau wa sekta binafsi watapewa kipaumbele kwa ajili ya kuzalisha Mbegu. Ujenzi wa mabwawa 14 yatakayokuwa na miundombinu ya umwagiliaji kwa matumizi ya kilimo na mifugo.

Hussein Bashe Mheshimiwa Hussein Bashe - Waziri wa Kilimo

Akifungua semina ya siku mbili iliyowahusisha wadau wa Sekta ya Umwagiliaji mjini Morogoro. Waziri Bashe ameendelea kusema kuwa utekelezaji wa kazi hiyo utakwenda sambamba na kuanzishwa kwa Ofisi za Umwagiliaji za Wilaya nchi nzima. Pamoja na kuajiri wasimamizi wa Skimu za umwagiliaji watakao husika kusimamia zoezi la ukusanyaji wa ada na tozo za umwagiliaji kwa uhakika.

Eneo lingine la kipaumbele kwa Waziri Bashe ni pamoja na kuwasaidia Wakulima Wadogo wadogo kupata Teknolojia bora za kilimo cha umwagiliaji kwa bei nafuu.  Ili waweze kupata tija na kuchangia ongezeko la mavuno katika sekta ya umwagiliaji. Zoezi hilo litawahusu pia Vijana wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amewataka watumishi wote wa tume ya Taifa ya Umwagiliaji  kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutimiza matarajio yaliyowekwa na serikali. Akiamini taasisi yake ina uwezo wa kutekeleza majukumu yaliyopangwa na serikali kwa wakati, ufanisi na ubora unaotakiwa katika kuhudumia wananchi.

Bw, Raymond MndolwaBw. Raymond Mndolwa - Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

“Nitamsapoti kila mtumishi aweze kutimiza wajibu wake, tumejipanga na lililopo mbele yetu tunaweza kulitekeleza”

Semina hiyo ya siku mbili imewashirikisha wadau mbalimbali. Ikiwemo sekta binafsi, Wakulima wadogo, Wataalam wa Benki, Vyama vya Ushirika, Wahandisi na Maafisa kilimo wa Wilaya ikiangazia namna ya kuboresha maeneo matatu muhimu katika kilimo cha umwagiliaji. Uzalishaji, huduma za  umwagiliaji na njia bora ya kukusanya Ada na Tozo za Umwagiliaji.