Habari

TUME YATILIANA SAINI NA WAKANDARASI MIKATABA 4 YA UJENZI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI

TUME YATILIANA SAINI NA WAKANDARASI MIKATABA 4 YA UJENZI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI
Apr, 28 2023

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetiliana saini mikataba 4 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na wakandarasi, yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 41 ikiwa ni utekelezaji wa bajeti ya mwaka wizara ya Kilimo ya mwaka 2022 – 2023. Akizungumza wakati wa   kutiliana saini makubaliano ya mikataba hiyo, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa anaishukuru serikali kwa kuwezesha tume ya umwagiliaji kutekeleza majukumu yake vema kutokana na fedha zilizoelekezwa kwenye miradi kutolewa kwa wakati huku akitoa angalizo kwa wakandarasi kuonyesha uzalendo wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa kujenga miundombinu kwa kiwango stahili.
Kwa upande wao baadhi ya wabunge walionufaika na miradi hiyo akiwemo mbunge wa jimbo la Korogwe Mjini Mhe.Dkt. Alfred Kimea, Mhe. Fransis Mtinga Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki (Mkalama) na Mhe. Jafari Chege Mbunge wa Rorya wamemshukuru rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza fedha za miradi ya umwagiliaji katika majimbo yao hatua itakayosaidia kuinua uchumi wa wakazi katika majimbo hayo, kupanua wigo wa kipato katika sekta ya kilimo, uhakika wa chakula na kuinua maisha ya wananchi kupitia miradi ya kilimo cha umwagiliaji.
Miradi inayotekelezwa katika wilaya hizo ni pamoja na ujenzi wa Skimu ya Mahenge - Korogwe (Tanga) yenye Hekta 480 kwa zaidi shilingi  Bilioni 1.85 mradi unaojengwa na mkandarasi M/S Gilco T Ltd, Bwawa la Msingi (Mkalama Singida)  litakalokuwa na Mita za ujazo Milioni 4 kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 34, linalojengwa na Mkandarasi M/S Nakuroi Investment Co Ltd, Skimu ya Iyombo - Tabora Manispaa yenye Hekta 500 kwa zaidi ya shilingi Bilioni 4.4. na Mkandarasi Ami Vai Ltd na Skimu ya Rabour iliyoko Rorya(Mara) yenye Hekta 650 kwa zaidi ya shilingi Milioni 987.2 inayojengwa na Mkandarasi M/S Isimila Company Ltd.