Habari

MAAGIZO YA NAIBU WAZIRI BASHE KWA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI

MAAGIZO YA NAIBU WAZIRI BASHE KWA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI
Nov, 26 2021

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe. Hussein Bashe (MB) ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia wahandisi wa wake wa mikoa kuainisha eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, na kusema kuwa ni ngumu kuwa na kilimo endelevu cha umwagiliaji kama hakuna mfumo endelevu wa kilimo hicho.

Naibu Waziri Bashe, ameyasema hayo jana jioni jijini Dodoma, alipokuwa katika kikao cha pamoja na wahandisi wa Umwagiliaji wa Mikoa na menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Bashe alisema kuwa, wahandisi wa Umwagiliaji nchini wanatakiwa kwenda kusajili skimu zote za kilimo ili kuweza kupata picha halisi, na kuzitambua skimu hizo pamoja na eneo lote linalofaa katika kilimo cha umwagiliaji. “Potential areas za miradi zitambulike, na za mabwawa zitambulike, tutenganishe miradi inayoweza kufanywa kwa ujenzi shirikishi yaani force account na miradi mingine.” Alisisitiza Bashe.

Aliendelea kusema kuwa, ni Lazima Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ijue inajenga hekta ngapi mpya za Umwagiliaji, pamoja na kuzifanyia matengenezo skimu nyingine, na kujiekea malengo ili kuweza kufikia lengo la ilani ya Chama cha Mapinduzi inayotaka hekta zaidi ya milioni moja na laki mbili(1,200,000)kumwagiliwa ifikapo mwaka 2025.

Akiongea kuhusu Mitambo iliyopo katika sekta ya kilimo cha Umwagiliaji na kumilikiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Naibu Waziri Bashe alisema, vifaa vyote vifanyiwe matengenezo na uanishwe ununuaji wa mitambo mipya.

Awali Naibu Waziri Bashe, aliagiza Tume hiyo kuwa na Muundo katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji utakaoonesha wahandisi wa umwagiliaji wa Wilaya nchini na alisisitiza swala zima la kuandaa budget halisi itakayokidhi mahitaji ya Ofisi hiyo.