Habari

Poland kusaidia Kilimo cha Umwagiliaji.

Poland kusaidia Kilimo cha Umwagiliaji.
Feb, 26 2019

NCHI ya Poland imesema inadhamiria kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo cha umwagiliaji nchini.

Akizungumza na wataalamu toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Balozi wa Poland nchini Bwana Krisyztof Buzalski amesema sekta ya kilimo cha umwagiliaji ni kati ya maeneo muhimu ambayo nchi yake imeona inaweza kushirikiana na Tanzania ili kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula hapa nchini.

Wataalamu toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji walipata fursa ya kumweleza Balozi Buzalski fursa zilizopo na mazingira bora ya uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kufuatia maelezo ya watalaamu hao Balozi Buzalski alionekana kuvutiwa na namna ambavyo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imejipanga kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza kilimo cha umwagiliaji nchini chini ya Mpango kabambe wa Umwagiliajihivyo kurahisisha nchi yake kusaidia.

Amesema Poland ni miongoni mwa nchi za barani Ulaya ambazo uchumi wake unategemea sana kilimo, hivyo Tanzania inaweza kujifunza mambo mengi katika sekta hiyo.

“Ninaamini ushirikiano wa nchi zetu hizi mbili katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji utaleta ufanisi mkubwa hususani eneo la teknolojia ya kisasa” Alisema Balozi Buzalski.

Akizungumzia kuhusu mikoa ambayo inakabiliwa na uhaba wa maji, Balozi alisema Poland inaweza kusaidia kupata mbadala wa kutatua kero hiyo, wakati katika maeneo yenye maji mengi, watahakikisha kuwa maji yanatumika kwa faida bila kupotea.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Dk. Eliakim Chitutu, amesema mazungumzo hayo na Balozi Buzalski yameweka msingi na kutoa mwanga yautekelezaji wa miradi mikubwa kwenye sekta ya kilimo cha umwagiliaji.

Chitutu amesema anaamini Poland inadhamira ya dhati ya kutaka kuinua sekta ya kilimo cha umwagiliaji na kwamba hatua itakayofuata ni wataalamu wakilimo cha Umwagiliaji nchini Poland kukutana na wenzao wa Tanzania ili kujadiliana kwa kina namna ya kupanga na kutekeleza miradi hiyo.