Habari

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATAKA WAKULIMA WA ZABIBU HOMBOLO KUILINDA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATAKA WAKULIMA WA ZABIBU HOMBOLO KUILINDA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI.
Jul, 14 2021

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakulima wa Zabibu katika shamba la kilimo cha umwagiliaji Hombolo, kuilinda miundombinu ya umwagiliaji isiharibiwe.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika shamba la Zabibu Hombolo kilomita 47 nje kidogo ya jiji la Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema miradi ya umwagiliaji ni ya gharama kubwa hivyo ni vema kuilinda kwa gharama zozote ili isiharibiwe ambapo pia amewapongeza wakulima wa Zabibu katika shamba hilo kwa jitihada zao katika kilimo hicho.

Waziri Mkuu Majaliwa amewahakikishia wakilima hao kuwa serikali ya awamu ya sita ipo pamoja nao ili kuhakikisha kilimo cha Zabibu kinapewa msukumo hivyo kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan ametuagiza kufuatilia kwa karibu kilimo cha Zabibu na ndio maana timu kubwa ya viongozi imekuja hapa lengo ni kuona changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.”

Aidha Majaliwa amewataka viongozi wote wanaohusika na masuala ya kilimo kufika mara kwa mara katika skimu hiyo kwa lengo la kuwasaidia wakulima wa Zabibu kufikia malengo yao.