Habari

Tume ya Taifa ya umwagiliaji imejiwekea mikakati ya kukusanya Shilingi Bilioni 30

Tume ya Taifa ya umwagiliaji imejiwekea mikakati ya kukusanya Shilingi Bilioni 30
Oct, 08 2021

Tume ya Taifa ya umwagiliaji imejiwekea mikakati ya kukusanya Shilingi Bilioni 30 kwa mwaka wa fedha 2021 – 2022 kwa lengo la kutunisha mfuko wa umwagiliaji wenye majukumu ya kukarabati na kujenga miundombinu ya skimu za umwagiliaji nchini.

Mkurugenzi wa tume ya taifa ya umwagiliaji Bw, Daudi Kaali, amesema katika kufanikisha mpango huo tume imewaleta pamoja wadau muhimu wa sekta ya kilimo kwa lengo la kujadiliana na hatimaye kupata mfumo bora,rahisi na wenye tija katika ukusanyaji wa tozo za umwagiliaji.

“ Miongoni mwa wadau walioshiriki ni Benki ya maendeleo ya kilimo ambapo wamewasilisha mapendekezo yao namna ya kugharamia sekta ya kilimo cha umwagiliaji ambapo wadau kutoka halmashauri na mikoa wamepata fursa ya kutoa ushauri na benki ya kilimo itayafanyia kazi na kupeleka serikalini kwaajili ya kufanyia kazi.”

Kaimu meneja uendelezaji Bw, Mohamed Mcheni amesema utaratibu wa ukusanyaji tozo umegawanyika katika makundi matatu, vyama vya wamwagiliaji watakusanya tozo za umwagiliaji kutoka mkulima mmoja mmoja kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa heka moja kwa msimu kwa zao hususan Mahindi na Mpunga huku tume ikiendelea kuzifanyia kazi bei za mazao mengine.

Utaratibu wa kukusanya tozo ya umwagiliaji ni kwamba viongozi wa vyama watatoa risiti kwa kila mkulima atakayetoa fedha zake na kisha wataziweka fedha hizo katika akaunti yao ambayo kwa kawaida huwa chini ya mkurugenzi na kisha mkurugenzi atahusika katika kuzigawanya fedha hizo ambapo asilimia 75 katika elfu 50 iliyokusanywa itabaki katika akaunti ya chama husika na asilimia 25 zitaingizwa katika mfuko wa umwagiliaji.