Habari

WANANCHI KIGOMA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KUPITIA BONDE LA LUICHE

WANANCHI KIGOMA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KUPITIA BONDE LA LUICHE
Jul, 14 2021

Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma hususan katika vijiji vya Kamara, Simbo, Machanzo, Nyomoli na Kasuku wanategemea kunufaika na kilimo cha umwagiliaji kupitia mradi mkubwa wa uendelezwaji wa bonde la Luwiche unaotegemea kuanza mapema mwakani.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi, Mkama Kimasa amesema kuwa Serikali imeshafanya makubaliano na Serikali ya Kuwait juu ya utekelezajji wa mradi huo na eneo la hekta elfu tatu ambazo zipo kwenye mkataba zinategemea kuendelezwa katika maana ya kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, na mchakato wa kutafuta mzabuni umeanza.

Mhandisi Kimasa amesema, mradi huo utagharimu kiasi cha fedha za mkopo zaidi ya shilingi Bilioni ishirini mpaka kumalizika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kamara moja ya kijiji kitakachonufaika na Mradi huo, Bw. Omary Katura akiongea kijijini hapo amesema, wananchi wa kijiji hicho wanategemea kupata mafanikio makubwa endapo mradi huo utatekelezeka kwakuwa wananchi wameshaukubali mradi huo, “Tunasubiria tuu Wizara na Taasisi husika waje kuanza ujenzi haraka kwa sababu na sisi wenyewe tumeshafika katika maeneo ambapo wanategemea kufanya ujenzi na tukajiridhisha kuwa hakuna matatizo sana ambapo changamoto ni ndogo tuu za kawaida ambazo ni njia za kupitisha vifaa hivyo mpaka maeneo ya site.” Alisema

Kwa upande wake Afisa Umwagiliaji wa Wilaya Hiyo Bwana Sudi Hussein amesema, kwa sasa wakulima wanalima kwa kutegemea msimu wa mvua na wanaweza kulima kwa vipindi viwili tofauti hivyo endapo mradi huo utafanikiwa wakulima wataweza kulima mara tatu kwa mwaka na kupata faida zaidi,

Mazao yanayolimwa kwa sasa katika Bonde hilo ni Mpunga, Mahindi na mazao mengine ya mbogamboga.