Habari

Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji Mbeya

Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji Mbeya
Apr, 01 2020

Na MwandishiWetu, Mbeya

UBORESHAJI wa miundo mbinu ya umwagiliaji mkoani Mbeya imeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 49,117 mwaka 2018 hadi kufikia hekta 71,890 mwezi Marchi 2020.

Akizungumza ofisini kwake Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoani Mbeya Elibariki Mwendo amesema uboreshwaji wa miundombinu hiyo umefanyika katika skimu za Mbaka na Katelantaba(Busokelo), Uturo ,Gwiri ,Igomelo, Mwendamtitu (Mbarali) na Mshewe (MbeyaVijiji).

Akifafanua Mhandisi Mwendo amesema baada ya uboreshaji wa miundo mbinu ya umwagiliaji kwa sasa eneo la umwagiliaji katika skimu ya Mbaka ni hekta 500, na Katelantaba eneo la umwagiliaji ni hekta 250 , wakati katika skimu ya Uturo eneo linalomwagiliwa ni hekta 900.

Ameongeza kuwa katika skimu ya Gwiri eneo linalomwagiliwa ni hekta 400, Igomelo ni hekta 312 wakati skimu ya Mwenda mtitu ina eneo la umwagiliaji lipatalo hekta 3000 na Mshewe Wilaya ya Mbeya Vijijini ina eneo la hekta 250.

Mhandisi Mwendo amesema kutokana na uboreshaji wa miundo mbinu ya umwagiliaji mkoani Mbeya, uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji umeimarisha kilimo cha umwagiliaji ambacho ndio kilimo cha uhakika, ambapo uzalishaji wa mazao ya chakula kama vile mpunga, mahindi na mboga umeongezeka, na hivyo kuinua kipato cha familia, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Aidha Mhandisi Mwendo amesema kutokana na serikali ya awamu yaTano kupitiaTume yaTaifa ya Umwagiliaji kuendelea kutenga fedha kwa ajili yakuboresha skimu za umwagiliaji ili kuhakikisha skimu hizo zinazalisha mazao ya chakula matunda na mbogamboga kwa mwaka mzima na hivyo kuwa na usalama wa chakula nchini.

Akiongea mapema, Afisa Kilimo Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoani Mbeya Bw. MnadiTaribo amesema Tume imeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa wakulima kama vile kilimo shaded cha mpunga,(System of Rice Intensification-SRI) ambacho hutumia maji kidogo na uzalishaji wake k wa zao la mpunga unakuwa mara mbili Zaidi ukilinganisha na kilimo kinachotumia maji mengi.

Akitoa mfano Taribo amesema katika Skimu ya umwagiliaji ya Madibirau uzalishaji wa zao la mpunga kwa kilimo cha kawaida (majimengi) hutoa tani 7.2 kwa hekta wakati kilimo shadidi (maji kidogo) huzalisha tani 9 .3 kwa hekta.

Skimu ya umwagiliaji ya Uturo uzalishwaji wa zao la mpunga kwa kilimo cha kawaida ni tani 5.7 kwa hekta wa kati kilimo shadidi huzalisha tani 13 kwa hekta,

Taribo ameongeza kuwa kilimo shadidi kinatumia maji kidogo kwa chini ya asilimia hamsini ukilinganisha na kilimo cha kawaida na uzalishaji wake ni mkubwa na kuwa na matumizi bora ya rasilimali maji.

Maboresho ya miundo mbinu ya umwagiliaji katika mkoa wa Mbeya kuanzia mwaka 2014 hadi 2020 yamegharimu Tshs.bilioni 3.2