Habari

WAHANDISI UMWAGILIAJI WAJENGEWA UWEZO KUBORESHA USIMAMIZI WA MIRADI

WAHANDISI UMWAGILIAJI WAJENGEWA UWEZO KUBORESHA USIMAMIZI WA MIRADI
Mar, 07 2024

Wahandisi umwagiliaji Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wamejengewa uwezo wa namna bora ya usimamizi wa miradi, elimu ya afya pamoja na usimamizi wa mikataba.

Akizungumza katika mafunzo hayo jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa ameeleza umuhimu wa mafunzo hayo kwa wahandisi ni kuhakikisha fedha zilizowekezwa katika miradi ya umwagiliaji zinaleta matokeo chanya na kutekeleza azma ya serikali kwa kuhakikisha  kilimo cha Umwagiliaji kinaleta tija kwa wakulima.

KWA upande wake Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Miundombinu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi mshauri. Kuyoya Fuko ambaye pia ni mwezeshaji katika mafunzo hayo ameeleza mambo ya msingi yatakayojadiliwa katika mafunzo hayo ni pamoja na kuwawezesha wahandisi wa umwagiliaji elimu ya kupima kazi zao, kudhibiti ongezeko la kazi pamoja na kujua sheria na kanuni katika kufunga miradi.

Mhandisi Fuko ameongeza kuwa sanjari na usimamizi wa miradi wahandisi hao watapewa elimu ya afya pamoja na usalama mahali pa kazi, pamoja na kujengewa uwezo wa kuboresha mahusiano kazini baina ya watumishi  wa Tume na jamii inayozunguka eneo la  mradi husika ili kushiriki katika utekelezaji wa miradi pamoja na kuilinda.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Yahya Amour amesema ili mradi uanzishwe ni lazima kuwepo na hatua za kusaini mikataba hivyo, elimu ya usimamizi wa mikataba utawezesha wahandisi hao kuzingatia ubora wa miradi kwa kufuata sheria na kanuni zinazowekwa katika mikataba kwa lengo la kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kuleta tija kwa wakulima na Taifa Kwa ujumla.

Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa wakulima na kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinakuza Pato la wakulima  na kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula.

Mwisho.