Habari

Wataalam Kilimo cha Umwagiliaji Nchini Wapigwa Msasa

Wataalam Kilimo cha Umwagiliaji Nchini Wapigwa Msasa
Jun, 30 2019

Imeelezwa kuwa Serikali kwa kushirikina na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan JICA kwa kupitia mradi wa kujengea uwezo wataalam nchini katika eneo la umwagiliaji imewapatia wahandisi na wataalam katika eneo la kilimo cha umwagiliaji mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo katika eneo la Mradi.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Usanifu na Utafiti Mhandisi Muyenjwa Maugo kutoka Tume ya Taifa ya umwagiliaji, ambapo Maugo alisema sambamba na hilo mradi pia umeendelea kutoamiongozo ikiwa ni pamoja na vitendea kazi vitakavyotumika katika ujenzi wa Miundombinu ya Umwagiliaji na upembuzi yakinifu ambapo ameeleza kuwa awali hakukuwa na muongozo katika skimu za miradi ya umwagiliaji jambo ambalo lilisababisha shughuli za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kutofanyika katika ubora unaostahili.

“Serikali inatumia rasimali nyingi kama vile fedha ili kuhakikisha miundombinu ya umwagiliaji inakuwa katika ubora unaostahili hivyo hatutaweza kuvumilia uendeshaji na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji usiofuata utaratibu na hatimaye kuwa chini ya kiwango.” Alisema Maugo.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uendeshaji na Mtunzo Bw. Anthony Nyarubamba alisema kuwa Uelelimishaji katika eneo la utunzaji wa miundombinu ya kilimo cha umwagilaji unaweza kuongeza tija katika eneo la uzalishaji wa chakula katika skimu nyingi za umwagiliaji nchini kwani muitikio kwa wakulima ni mkubwa mno. Akitolea mfano wa skimu ya kilimo cha umwagiliaji cha Igomelo Mkoani Mbeya ,Bw. Nyarubamba amasema kabla ya bei ya kitunguu kuharibika mkulima wa zao hilo alikuwa akipata takribani shilingi miloni Arobaini (40) kwa mwaka.

Aidha Bw. Nyarubamba amesema ili Nchi iweze kuingia vizuri katika uchumi wa Viwanda kilimo cha umwagiliaji kikitumika vizuri Nchi inaweza kupata malighafi za viwanda na kujipanga kulingana na masoko kutokana na upatikanaji wa mazao ya kutosha.