Mkoa wa Mtwara

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,

Mkoa wa Mtwara,

S.L.P 671,

MTWARA.

TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI

TAARIFA YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MKOANI MTWARA

Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa 26 ya Tanzania bara uliopo kusini mwa Tanzania ambao una eneo la hekta 1,672,000. Kiutawala mkoa umegawanywa katika wilaya tano (5) za Mtwara, Masasi, Newala, Nanyumbu na Tandahimba. Mkoa una mamlaka za serikali za mitaa tisa (9) ambazo ni halmashauri ya manispaa Mtwara Mikindani, halmashauri ya wilaya Masasi, halmashauri ya wilaya Mtwara, halmashauri ya wilaya Newala, halmashauri ya wilaya Tandahimba, halmashauri ya wilaya Nanyumbu, halmashauri ya mji Newala, halmashauri ya mji Masasi na halmashauri ya mji Nanyamba.

Mkoa una eneo lipatalo hekta 1,421,200 zinazofaa kwa kilimo ambapo eneo lipatalo hekta 468,996 linatumika kwa uzalishaji wa mazao. Eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 16,644.50, hata hivyo eneo linalomwagiliwa ni hekta 3848.6. Vyanzo vya maji ya umwagiliaji ni mito, chemchem na maji ya ardhini. Mkoa una skimu za umwagiliaji ishirini na sita (26), skimu zilizoendelezwa kumi (10) zinazomwagiliwa hekta 1,337.8 na skimu za asili kumi na sita (16) zinazomwagiliwa hekta 2,510.8. Skimu moja pekee kwenye mkoa imesajiliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Idadi na aina ya skimu kwa wilaya ni kama ifuatavyo: Mtwara skimu tatu (3) zimeendelezwa na nane (8) za asili; Masasi skimu mbili (2) zimeendelezwa; Newala skimu mbili (2) zimeendelezwa na mbili (2) za asili; Nanyumbu skimu mbili (2) za asili; Tandahimba skimu nne (4) zimeendelezwa na mbili (2) za asili. Mazao yanayolimwa kwenye skimu za umwagiliaji ni mpunga na mboga mboga, wastani wa mavuno ya mpunga kwa hekta kwenye skimu zilizoendelezwa na asili ni tani tano (5) na tani mbili nukta tatu (2.3) mtawalia. Mazao mengine yanayolimwa katika mkoa wa Mtwara ni mahindi, viazi vitamu, muhogo, kunde, mbaazi, njugu, mtama, choroko, korosho, karanga na ufuta.