Mkoa wa Njombe

Ofisi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Njombe inahudumia Halmashauri za Wilaya nne (4) na Halmashauri za Mji mbili (2) yaani ni Ludewa DC, Makete DC, Njombe DC, Wanging’ombe DC, Njombe TC na Makambako TC. 
Mkoa wa Njombe una jumla ya Hekta 1,090,000 zinazofaa kwa kilimo kati ya hizo ni Hekta 21,836 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Eneo linalomwagiliwa katika Mkoa wa Njombe mpaka sasa ni hekta 5,652. 

Mkoa wa Njombe unajumla ya Skimu za Umwagiliaji 46 ambazo skimu 4 zipo Halmashauri ya Wilaya Ludewa, skimu 8 zipo Halmashauri ya Wilaya Makete, skimu 7 zipo Halmashauri ya Wilaya Njombe, skimu 16 zipo Halmashauri ya Wilya Wanging’ombe, skimu 6 zipo Halmashauri ya Mji Njombe na skimu 5 zipo Halmashauri ya Mji Makambako. Kati ya hizo skimu 15 zimeboreshwa miundombinu ya umwagiliaji na skimu 31 ni za asili. Skimu nne (4) zimesajiliwa kwenye mfumo wa tume ya Taifa ya Umwagiliaji na skimu saba (7) zimesajiliwa chini ya Maendeleo ya Ushirika. Mkakati uliopo ni kuhakikisha tunapita kwenye skimu zote za umwagiliaji ambazo hazijasajiliwa kwenye mfumo wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kutoa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kusajili skimu zao kwenye mfumo wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji mwaka mzima kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji ni Mto Fukurwa, Mto Unyuguru, Mto Madege, Mto Chimala, Mto Balali, Mto Mtitafu, Mto Halali, Mto Kihanga, Mto Mpeng'o, Mto Ng'engemala, Mto Mbukwa, Mto Ruhuhu, Mto Nyangundi na Mto Ruaha.
Mazao makuu yanayolimwa kwenye skimu za umwagiliaji ni Mpunga, Mahindi, Nyanya, Vitunguu, Viazi mviringo, Mboga za majani, Maharage, Parahichi na Chai. Wastani wa uzalishaji wa zao la Mpunga ni tani 3 kwa hekta, Mahindi ni tani 5 kwa hekta, Nyanya ni tani 3 kwa hekta, Vitunguu ni tani 4.5 kwa hekta, Viazi mviringo ni tani 12 kwa hekta, Mboga za majani ni tani 12 kwa hekta, Maharage ni tani 4 kwa hekta, Parachichi ni tani 18 kwa hekta na Chai ni tani 3.58 kwa hekta.