Mkoa wa Rukwa

Mkoa wa Rukwa ulianzishwa mwaka 1974 kwa kumega sehemu ya Mikoa ya Tabora na Mbeya. Mkoa huu upo kati ya Latitudo 70 – 90 Kusini mwa Ikweta na Longitudo 30 – 320 Mashariki mwa Grinwichi. Mkoa unapakana na Mikoa ya Katavi upande wa Kaskazini na Songwe upande wa Kusini Mashariki. Aidha, unapakana na nchi za Zambia upande wa Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa Magharibi. Mkoa una eneo la kilomita za mraba 27,765,  kati ya hizo Kilomita za mraba 22,844 (82.3%) ni za nchi kavu na Kilomita za mraba 4,921 (17.7%) ni za maji.

Muundo wa Mkoa Kiutawala

Mkoa una jumla ya Wilaya tatu (3) ambazo ni Sumbawanga, Kalambo na Nkasi na Halmashauri nne (4) ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri za Wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo. Aidha, ndani ya Mkoa kuna Mamlaka za Miji Midogo ya Namanyere Wilayani Nkasi na Laela Wilayani Sumbawanga. Yapo majimbo matano (5) ya Uchaguzi ambayo ni: Sumbawanga Mjini na Kwela – Wilaya ya Sumbawanga; Kalambo – Wilaya ya Kalambo; Nkasi Kusini na Nkasi Kaskazini – Wilaya ya Nkasi.Mkoa una Tarafa 16, Kata 97, Vijiji 339, Vitongoji 1,817 na  Mitaa 165.

  Idadi ya Watu

Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Mkoa wetu ulikuwa na idadi ya Wakazi wapatao 1,004,539 (Wanawake  517,228 na Wanaume 487,311). Mkoa una ongezeko la watu la wastani wa asilimia 3.2. kwa mwaka. Katika mwaka 2020 Mkoa unakadiriwa kuwa na idadi ya Wakazi wapatao 1,270,049 (Wanawake 654,075 na Wanaume 615,974).

Hali ya Hewa

Mkoa una hali ya hewa ya Kitropiki ambapo wastani wa joto ni Sentigredi 13 katika baadhi ya maeneo (kwa miezi ya Juni na Julai) hadi Sentigredi 27 (kwa miezi ya Oktoba na Desemba). Mkoa una Mvua za kutosha za wastani wa milimita 800 hadi 1,300 kwa mwaka, kuanzia mwezi  Novemba hadi Mei. Kiangazi ni mwezi Juni  hadi Oktoba.

FURSA ZA UMWAGILIAJI KATIKA MKOA

 

Katika mkoa wa Rukwa kuna fursa kubwa aina tatu za umwagiliaji,  ambazo ni;

-Ardhi kubwa yenye rutuba linalofaa kwa kilimo cha  umwagiliaji

-Upatikanaji wa Rasili mali maji

(Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa ,uwepo wa mito mikubwa kama mto momba)

-Upatikanaji wa soko

 

 

ENEO LINALOFAA KWA UMWAGILIAJI

 

Mkoa wa Rukwa hadi sasa unajumla ya Skimu  za Umwagiliaji 56 zilizotambuliwa zenye ukubwa wa Hekta 67,401 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hata hivyo juhudi za kuendelea kuyatambua maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji zinaendelea,Hekta 7250  sawa na 10.8% ya eneo lote linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji zimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu bora ya Umwagiliaji. Hekta 1,050 zimeendelezwa na kampuni ya   EMPIEN Ltd kwa kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji. Pamoja na hilo tuna mabonde makubwa yanayohitaji uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya umwagiliaji kama bonde la Maleza lenye zaidi ya hekta 7500 (Mto Momba),bonde la kilyamatundu(Mto Momba) lenye ukubwa wa hekta 15,000 ,bonde la Legezamwendo lenye ukubwa wa hekta 5500(Mto Momba), na bonde la mto Lwafi lenye ukubwa wa hekta 3200(mwambao wa ziwa Tanganyika)

 

UPATIKANAJI WA RASILI MALI MAJI

Mkoa wa Rukwa umebarikiwa kuwa na vyanzo vya uhakika wa maji safi yasiyo na chumvi kama vile Ziwa Tanganyika,Ziwa Rukwa na uwepo wa mito mikubwa kama vile mto momba na idadi kubwa ya mito midogomidogo inayotililisha maji kwa kipindi chote cha mwaka hivyo kama mabonde ya mito hiyo yakiendelezwa kutakuwa na uhakika wa kulima mala mbili kwa mwaka na kuongeza usalama na uhakika wa chakula.

 

UHAKIKA WA MASOKO YA MAZAO

 

Mkoa wa Rukwa umepakana na nchi ya Zambia na Kongo pamoja na maeneo ya kanda ya ziwa ambayo yana uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo yatokanayo na kilimo cha umwagiliaji ( mpunga, mahindi, mihogo, maharage na mbogamboga). kutokana na hilo ni fursa kwa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji kupata soko lenye tija na la uhakika.

 

SKIMU ZA UMWAGILIAJI ZILIZOENDELEZWA KWA FEDHA ZA SERIKALI.

Kupitia programu za DIDF, DADPS na SSIDP kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2008/09 hadi mwaka wa fedha 2016/2017 Mkoa ulipokea Jumla Shilingi 5, 896, 955,000/=kutoka Serikali  Kuu, fedha hizo zilizotumika katika kuendeleza Skimu sita za Umwagiliaji  kwa kujenga miundombinu ya msingi ya umwagiliaji. Skimu zilizonufaika ni pamoja na Sakalilo, Katuka, Ng’ongo, Singiwe, Katongolo/lwafi na Ulumi.

Kwa mwaka wa fedha 2022/2023  Mkoa unatarajia kutekeleza ujenzi wa skimu ya  umwagiliaji wa Ilemba wenye hekta 1650  ikiwa ni pamoja na kujenga bwawa na miundombinu yote ya mashambani.