Karibu
Kwa niaba ya Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Menejimenti na Watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ninayo furaha kuwakaribisha kwenye tovuti yetu.
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilianzishwa kwa Sheria ya Umwagiliaji Namba 4 ya mwaka 2013 ikiwa ni Idara inayojitegemea chini ya Wizara yenye dhamana ya umwagiliaji. Tangu kuanzishwa kwake, Tume imefanya juhudi kubwa katika kuendeleza umwagiliaji nchini Tanzania.
Tuna dira nzuri inayoeleza tunavyotaka kuwa - Tume endelevu ambayo inatoa msukumo wa kubadili kilimo kuwa sekta imara na ya ushindani nchini kwa kutoa huduma bora na za gharama nafuu na kuhakikisha kuwa umwagiliaji unazingatia uzalishaji wa mazao unaozingatia mabadiliko ya tabia nchi ili taifa lijitegemee kwa chakula na kuongeza kipato ikiwemo upatikanaji wa mali ghafi kwa ajili ya uchumi wa viwanda. Ninajivunia utekelezaji wa majukumu yetu na ninaahidi kuwa tutatimiza ahadi zetu kwa njia endelevu na kwa uwajibikaji huku tukizingatia mahusiano ya Maji-Nishati-Chakula pia hifadhi ya Mazingira.
Tunatekeleza majukumu yetu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo taasisi binafsi na umma katika juhudi za kuboresha kilimo cha umwagiliaji na kuhamasisha matumizi ya zana zitumiazo maji kwa ufanisi ili kuhakikisha uzalishaji wa mazao hata wakati wa upungufu wa maji kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Tuna wataalamu waliobobea na ambao ninaamini wanatupa uwezo tulionao na ambao tunawategemea kwenye mafanikio yetu. Ahsante kwa kutembelea tovuti yetu na ni matarajio yetu kuwa tutafanya kazi pamoja na kushirikiana. Karibu sana!
Bw. Raymond William Mndolwa
MKURUGENZI MKUU