Habari
DKT. NINDI ATETA NA MENEJIMENTI YA TUME

š NIRC Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa juhudi inazofanya katika utekelezaji miradi ya Umwagiliaji nchini.
Dkt. Nindi amesema hayo leo Ijumaa Mei 9, 2025 alipotembelea ofisi za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji jijini Dodoma na kufanya kikao na menejimenti ya Tume.
Amewasihi kuendelea na jitihada wanazofanya katika kuboresha sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji kwani nchi ina maeneo makubwa yanayofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji.
Amesema lengo la Serikali ni kuboresha mifumo ya uzalishaji nchini sio uzalishaji wa mazao ya kilimo pekee, bali ni pamoja na uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi, hivyo Tume ipo katikati kuhakikisha mazao yote yanazalishwa.
Amesema Tume ina fursa kubwa mbali na kuanza na mazao ya kilimo pia inaweza kuunganisha mazao mengine yanayotokana na mifugo na uvuvi.
Aidha, Dkt. Nindi amesema maeneo mengi ambayo miradi ya umwagiliaji inatekelezwa, yatavutia watu wengi kwa kuweka makazi, kutokana na uwepo wa shughuli za binadamu, hivyo matumizi ya ardhi katika maeneo hayo yanaweza kuchangia uharibifu wa miundombinu ya Umwagiliaji, ikiwemo mabwawa.
Dkt. Nindi amesisitiza kuwa Tume ina wajibu wa kushirikisha maafisa ardhi wa maeneo husika, ili kuepuka athari zinazoweza kutokea katika skimu kutokana na shughuli za kila siku za binadamu.
Dkt. Nindi ameongeza kuwa Tume kuimarisha mifumo ya kidigitali, kwa lengo la kurahisisha zoezi la ukusanyaji ada ya huduma za Umwagiliaji.
Dkt. Nindi pia amesema umuhimu wa Kilimo cha Umwagiliaji ni zaidi ya usalama wa chakula kwani matokeo yake ni kuwa na usalama wa chakula, uhuru wa chakula na kuwa na kilimo cha kibiashara ambacho kitakuza uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Maria Itembe amesema tayari Tume imeanza jitihada za kuyalinda maeneo yanayotumika kwa shughuli za kilimo cha Umwagiliaji ili kudhibiti athari zinazoweza kuchangia uharibifu wa miundombinu na shughuli za kilimo kwa ujumla.
Sanjari na hayo Dkt. Nindi amehimiza ushirikiano kwa menejimenti katika utekelezaji wa majukumu ya Tume ili kuleta tija na kuhakikisha azma ya serikali inafikiwa kwa kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula, kupitia kilimo cha Umwagiliaji.