Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

WAHANDISI NIRC WAJENGEWA UWEZO KUIMARISHA USALAMA WA MABWAWA


📍  NIRC Iringa. 

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea na mafunzo ya usimamizi wa mikataba na utafiti wa miamba, kwa wahandisi, wasimamizi wa miradi (Project Managers), Menejiment na wataalamu wa kada mbalimbali ili kuhakikisha miundombinu ya mabwawa inayojengwa nchini inakuwa imara na salama.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Miundombinu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Leopold Runji, amesema utafiti wa miamba ni hatua muhimu inayohakikisha bwawa linajengwa mahali sahihi na kudumu kwa zaidi ya miaka 50 kama ilivyosanifiwa.

"Lengo ni kupata bwawa imara ambalo halitaleta madhara kwa wakazi au watumiaji. Tumefahamu kuwa bwawa linaweza kupasuka au kuvujisha maji kama utafiti wa miamba haukufanyika kwa kina.

"Mafunzo haya yamewapa wahandisi wetu uwezo wa kusimamia usanifu na ujenzi, lakini pia kukagua tafiti zinazoletwa na washauri waelekezi (consultants)," amesema Mhandisi Runji.

Mhadisi Runji amebainisha kuwa kwa sasa NIRC inasimamia ujenzi wa mabwawa zaidi ya 16 ambayo yanatarajiwa kukamilika na kuanza kujaa maji kati ya mwezi Machi na Mei mwaka huu, hivyo usimamizi makini unahitajika kulinda thamani ya fedha ambazo Serikali imewekeza.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka wa kutatua changamoto za kiufundi wanazokutana nazo maeneo ya kazi.

Mhandisi Theresia Edward Sule, ambaye ni mhandisi msaidizi wa mradi wa skimu ya Itete, amesema mafunzo hayo yamempa mwanga mpya wa jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya mienendo ya mito (river channels) ambayo huathiri usalama wa miundombinu ya kuvuna maji (intake).

Naye Mhandisi Abdallah Mahundi amebainisha kuwa elimu ya utafiti wa miamba imewaongezea weledi wa kutambua aina za miamba na vipimo (tests) vinavyohitaji misingi (foundation) imara ya miradi ya Umwagiliaji inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwajengea uwezo wa ndani wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya ufuatiliaji wa karibu wa miundombinu ili kuzuia upotevu wa maji na kuhakikisha usalama wa jamii inayozunguka miradi hiyo.