Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

MAKUBALIANO YAIBUA MATUMAINI MAPYA KWA WAKULIMA MAGOZI


šŸ“Magozi, Iringa Vijijini

Baada ya kipindi kirefu cha changamoto za uendeshaji na uharibifu wa miundombinu ya Umwagiliaji, wakulima wa skimu ya Magozi sasa wanaanza kuona mwanga mpya kufuatia kusainiwa kwa makubaliano rasmi yatakayobadilisha namna wanavyosimamia na kunufaika na kilimo chao. Hatua hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wakulima wanaotarajia kuona mabadiliko ya kweli katika uzalishaji na maisha yao ya kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Petro Sarwat amesema hatua hiyo ni matokeo ya juhudi za makusudi za Serikali kuhakikisha miundombinu ya umwagiliaji inakuwa endelevu. Ameeleza kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu, lakini changamoto imekuwa ni utunzaji wake. “Kupitia makubaliano haya, sasa kila upande umeelewa wajibu wake ili kuhakikisha miundombinu inadumu na kuongeza tija kwa wakulima wa sasa na vizazi vijavyo,” amesema.

Kwa upande wa wataalamu, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Iringa, Peter Akonay, amebainisha kuwa mkataba huo utaimarisha uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa shughuli za skimu. Ameeleza kuwa Tume kupitia ofisi zake za mkoa na wilaya itahakikisha changamoto zote zinashughulikiwa kwa wakati, huku akitaja pia uwekezaji mkubwa unaoendelea wa zaidi ya kilomita 25 za mfereji mkuu na miundombinu mingine itakayorahisisha upatikanaji wa maji mashambani.

Kwa wakulima, hatua hiyo imekuwa chachu ya matumaini mapya. Vicent Msega, mkulima katika skimu hiyo, amesema makubaliano hayo yamewafumbua macho kuhusu haki na wajibu wao, hasa katika kulinda rasilimali zao. “Sasa tunaelewa thamani ya mkataba na namna utakavyotusaidia kulinda ardhi na miundombinu yetu. Hii ni hatua kubwa kwa maendeleo yetu,” amesema.

Naye Kasimba Amani Simba, mkulima ambaye alishiriki mafunzo yaliyotangulia, ameeleza kuwa mkataba huo umejenga msingi mpya wa uwajibikaji na ushirikiano kati ya Serikali na wakulima. Amesisitiza kuwa tofauti na hapo awali, sasa kuna mwongozo unaoeleweka unaoainisha majukumu ya kila upande, jambo litakalosaidia kuondoa mkanganyiko na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa skimu.

 

Hatua hiyo ya kusainiwa kwa makubaliano imefikiwa baada ya wakulima na viongozi wa skimu ya Magozi kupatiwa mafunzo maalum ya uendeshaji, usimamizi na matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji, yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na mshauri elekezi INCATEMA kupitia mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula, yakilenga kuimarisha uendelevu wa miundombinu na kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo.

slot gacor