Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

MKURUGENZI MKUU WA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI ASHIRIKI KIKAO CHA BARAZA LA RAIS DKT SAMIA LA USHAURI WA KILIMO NA CHAKULA


NIRC Dodoma.

 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, ameshiriki katika kikao cha Baraza la Kumshauri Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu Utekelezaji wa Masuala ya Kilimo na Chakula (PAC-AF), kilichofanyika jijini Dodoma, chini ya  Mwenyekiti, ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda.

Kikao hicho kimekutanisha viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kimkakati kuhusu maboresho ya sekta hizo nchini. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Pinda amesisitiza haja ya kuwapo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara hizo mbili ili kufanikisha mahitaji ya wadau zaidi ya 1,570, ambao Baraza limekutana nao katika kanda mbalimbali; wakiwemo wadau wa sekta binafsi.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amebainisha kuwa kilimo kimeendelea kuwa moja ya vipaumbele vikuu vya Serikali. Amesema uwekezaji mkubwa uliyofanywa na Serikali,  umechochea ongezeko la bajeti ya Wizara hiyo, kutoka Shilingi bilioni 294 hadi kufikia zaidi ya Shilingi trilioni 1.2, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Waziri Chongolo amefafanua kuwa, tija imekuwa msingi wa uzalishaji kwa sasa, hususan katika eneo la Umwagiliaji, ambapo asilimia 60 ya bajeti ya Wizara imeelekezwa kwenye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Amesema kupitia bajeti hiyo, zaidi ya miradi 740 ya umwagiliaji imepangwa kutekelezwa nchi nzima ili kuimarisha usalama wa chakula.

Aidha, Waziri amebainisha kuwa Serikali imefanikiwa kupata masoko 14 nje ya nchi kwa ajili ya mazao ya viazi na matunda.Ameongeza kuwa fursa hizo zinahitaji uwekezaji mkubwa katika mifumo ya usafirishaji, uhifadhi, pamoja na teknolojia za kisasa za ukaushaji ili kukidhi vigezo vya kimataifa.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali za kisekta.