Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

SERIKALI YAIMARISHA USIMAMIZI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI KWA MFUMO WA WASHAURI ELEKEZI


 

📍 Nirc: Dodoma 

Serikali imeendelea kusisitiza uwajibikaji, ufanisi na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji , kupitia kikao kazi kilichowakutanisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, Menejimenti ya Tume, wahandisi wa mikoa, wakandarasi pamoja na washauri elekezi.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Bw. Gerald Mweli amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya Umwagiliaji , ambapo takribani asilimia 30 ya bajeti ya Wizara ya Kilimo inaelekezwa katika miradi ya Umwagiliaji . Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unalenga kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia uhakika wa maji, huku akitaka miradi yote kusimamiwa kwa ufanisi ili kuhakikisha “value for money” inapatikana.

 Aidha, ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika na ubadhirifu au kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, amesema Tume imejipanga kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora na tija, ambapo mfumo mpya wa usimamizi kupitia washauri elekezi utaongeza ufanisi na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani. 

Amebainisha kuwa baadhi ya miradi itasimamiwa na washauri wa ndani huku mingine ikisimamiwa na wa nje, hatua inayolenga kukuza utaalamu na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa miradi.

Kwa upande wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwakilishi wake Bw. Ipyana A Mlilo amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa mikataba, akieleza kuwa miradi yenye thamani kubwa inapitiwa na ofisi hiyo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu.

Kwa upande wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), mwakilishi wake Bw.Abraham J Kaaya amesisitiza kuzingatiwa kwa maadili ya taaluma, usajili halali wa wataalamu na miradi pamoja na kuhakikisha usalama wa wananchi na watumiaji wa miundombinu hiyo.

Vilevile upande wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), mwakilishi wake Bw. Meleck J Mwano amesisitiza ufuatiliaji wa kazi za ukandarasi na kutoa wito wa kuongezwa kwa fursa za miradi kwa wakandarasi wa ndani ili kuwawezesha kujenga uwezo na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta.

Kikao hicho pia kimeweka mkazo katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tume, washauri elekezi na wakandarasi, kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa miradi, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kuleta tija katika maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa taifa kwa ujumla.

slot gacor