Habari
WAZIRI CHONGOLO, TUME WATETA NAMNA BORA YA KULETA MATOKEO MIRADI YA UMWAGILIAJI
📍Dodoma
WAZIRI wa Kilimo Daniel Chongolo, Menejimenti ya Wizara,Bodi ya Uongozi na Menejiment ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekutana na kujadili hatua ya utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji na namna bora ya miradi hiyo kuleta matokeo.
Katika kikao kazi hicho Waziri Chongolo, ameitaka Tume kuongeza ufanisi katika miradi inayotekelezwa ili tija ipatikane zaidi kwa wakulima na kuwapo kwa uhakika wa usalama wa chakula nchini.
Amesema, anaridhishwa kwa kiasi kikubwa na namna Tume inavyotekeleza majukumu yake katika kusimamia na kuendeleza miradi ya Umwagiliaji, akibainisha kuwa sekta hiyo ni mhimili muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Taifa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutekeleza miradi kwa wakati pamoja na kuongeza uwekezaji katika miradi midogo ya Umwagiliaji ili kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa gharama nafuu. Amesema hatua hiyo italeta matokeo makubwa na ya haraka kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Tunajadili kutafuta matokeo. Tuzingatie tumetoka wapi kabla ya miradi kuanza, tuko wapi na tunaelekea wapi kwa kuzingatia upatikanaji wa tija inayoenda kuongeza pato kwa mkulima; kuongeza ajira na uzalishaji wa mazao,” amesisitiza Waziri Chongolo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Dkt. Richard Masika, amesema Tume imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na iko tayari kuyatekeleza kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Amefafanua kuwa Tume itaendelea kuimarisha uelewa kwa wananchi kuhusu miradi inayotekelezwa ili kuhakikisha wananufaika kikamilifu, sambamba na kuweka mikakati madhubuti ya kukamilisha miradi kwa kuzingatia makundi mbalimbali, ikiwemo miradi inayohitaji kukamilishwa kwa haraka, ya kati pamoja na miradi ya kimkakati ya muda mrefu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, amesema Tume itaendelea kufanya kazi kwa weledi na kujituma katika kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Ameongeza kuwa Tume itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia malengo ya kitaifa, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha maisha ya wakulima na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mndolwa amesisitiza kuwa, mipango ya miradi ya umwagiliaji imezingatia ushirikishwaji na utoaji wa elimu kwa wakulima wa eneo husika la miradi; ujenzi wa miundombinu inayoongeza uzalishaji kwa wakulima ili kuwa na matokeo chanya na yenye tija kwa muda mrefu.
Viongozi walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo; Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo; Mha. Athumani Kilundumya, Naibu Katibu Mkuu (Umwagiliaji na Zana za Kilimo); na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo.

