Habari
NIRC, INKATEMA ZAUNGANISHA NGUVU KUWANOA WASIMAMIZI WA SKIMU ZA UMWAGILIAJI
📍NIRC Dodoma.
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewataka wataalamu wanaoshiriki, mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo ili kukamilisha utoaji elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP-PforR), hususani katika kukamilisha mkataba wa Uendeshaji, Usimamizi na Matunzo ya miundombinu ya Umwagiliaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Maria Itembe, amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya taasisi pamoja na maelekezo ya Bodi ya Tume, ambayo imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mikataba kati ya wakulima na Serikali ili kuongeza thamani ya miradi inayotekelezwa iweze kuishi kwa muda mrefu.
_1776425038.jpeg)
Amesema kiu ya Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa na Bodi ya Uongozi ya NIRC ni kuona wataalamu wa Tume na wanufaika wa miradi hiyo wanatambua umuhimu wa kutunza, kusimamia na kuendesha miradi hiyo kwa ushirikiano hali ambayo itachochea ulipaji wa ada ya Huduma za Umwagiliaji kwa ufanisi.
“Mafunzo haya, yanayotekelezwa chini ya mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania-TFRP, yanalenga kuwajengea uwezo mameneja wa skimu kuwa wakufunzi watakaowawezesha wakulima kuendesha skimu kwa ufanisi na kuingia mikataba rasmi ya uendeshaji, usimamizi na matunzo ya miundombinu ya Umwagiliaji hivyo muwe tayari kujifunza na kwenda kutafanyia kazi.
“Kupitia mafunzo haya, tunaamini mtakwenda kutimiza matarajio ya Tume kwa kuhakikisha wakulima wanaelewa wajibu wao na kuingia mikataba itakayosaidia kutunza miundombinu na kuongeza tija. Hatutaki tena kujenga miundombinu na kuiacha iharibike bila matokeo,” alisema Itembe.
Amesisitiza kuwa uwepo wa mikataba hiyo utasaidia kuweka uwajibikaji kwa pande zote mbili, huku akieleza kuwa baadhi ya changamoto zilizokuwepo ni pamoja na wakulima kutotambua wajibu wao katika kuchangia na kutunza miundombinu hiyo.
“Serikali inawekeza fedha nyingi kujenga miradi ya Umwagiliaji, hivyo ni muhimu kuhakikisha uwekezaji huo unazaa matunda. Kupitia mikataba, kila upande utatambua wajibu wake na kutekeleza ipasavyo,” ameongeza.
Aidha, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa chachu ya mabadiliko kwa kutumia maarifa watakayopata kuwafundisha wakulima wengi zaidi ili kufikia skimu nyingi zaidi nchini.

Kwa upande wake, Jackson Nicholaus Masakia kiongozi wa timu kutoka upande wa wataalam washauri wa INKATEMA, ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tume na wataalam hao ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya programu hiyo yanafikiwa.
“Tunaishukuru NIRC kwa ushirikiano mkubwa. Mafanikio ya programu hii yanategemea ushirikiano wetu sote, kwani lengo ni kuona tunafanikisha utekelezaji wake kwa vitendo katika ngazi ya skimu,” alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na mafunzo ya darasani, utekelezaji halisi utafanyika shambani, ambapo washiriki watapata uzoefu wa moja kwa moja katika kusimamia skimu.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dkt. Paul Mwinuka, amesema ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wataalam umeongeza ufanisi wa mafunzo na kuwajengea washiriki uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika skimu.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza kwa vitendo masuala ya upangaji wa matumizi ya maji , pamoja na kufanya mahesabu ya mahitaji ya maji kwa mazao, usmamizi bora wa skimu za Umwagiliaji na matumizi sahihi ya rasilimali maji, hatua muhimu katika kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali maji na kuongeza tija ya kilimo.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kwa siku 16, yakilenga kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya Umwagiliaji na kuchochea maendeleo ya kilimo endelevu nchini.


