Habari
WAKULIMA SAME, NIRC WATETA NAMNA BORA YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI
📍NIRC Same, Kilimanjaro.
Wakulima wa skimu ya Umwagiliaji Kihurio iliyopo vijiji vya Uzambara na Kankokoro, Kata ya Kihurio, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa mafunzo ya uendeshaji, usimamizi na matunzo ya miundombinu ya Umwagiliaji ili kuongeza tija ya uzalishaji.
Mafunzo hayo yaliyotolewa yamelenga kuwajengea uwezo wakulima na viongozi wao katika kusimamia skimu yenye jumla ya hekta 497 za eneo la Umwagiliaji.
Diwani wa Kata ya hiyo, Mariani Abdurrahman, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia wakulima na viongozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
_1774424815.jpeg)
Amesema, awali baadhi ya vyama vya Umwagiliaji vilikumbwa na changamoto ya uelewa mdogo hali iliyosababisha kushindwa kusimamia rasilimali kwa manufaa ya wanachama.
“Kuanzia sasa kila mmoja anajua wajibu wake na atakayefanya makosa atakuwa amefanya kwa makusudi kwa sababu elimu imetolewa ya kutosha,” amesema Mariani.
Afisa Maendeleo ya Jamii Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Heaven Jesse, amesema ushirikiano kati ya wakulima na wataalamu ni muhimu katika kuhakikisha miundombinu inasimamiwa kwa ufanisi.

Amesema, kamati za skimu zinapaswa kufanya kazi kwa karibu na wataalamu ili kuhakikisha maamuzi yote yanazingatia ushauri wa kitaalamu, hususan katika matengenezo ya mifereji.
“Tunasisitiza mkafanye kazi bega kwa bega na wataalamu ili kuepuka makosa na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali maji,” amesema Jesse.
Mkulima wa skimu hiyo, Abdallah Habib, amesema licha ya mafanikio ya mradi huo bado kuna changamoto ya mifereji ya upili na utatu ambayo inahitaji kuboreshwa ili kuhakikisha maji yanafika katika mashamba yote.
Amesema bila maboresho ya mifereji hiyo, uwekezaji unaofanyika kwenye mfereji mkuu unaweza usilete matokeo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo, mkulima Mwanaisha Zayumba, amesema changamoto ya miundombinu ya barabara katika eneo la skimu bado ni kikwazo kwa wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Amesema hali hiyo inaongeza gharama za uzalishaji na kupunguza faida kwa wakulima, hivyo kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha miundombinu hiyo ili kuongeza tija ya kilimo.

