Habari
UREJESHAJI MTO LUKOSI, KWAFUFUA MATUMAINI KILIMO CHA UMWAGILIAJI RUAHA MBUYUNI
📍 Ruaha Mbuyuni, Kilolo
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imefanya mapitio ya maendeleo ya mradi wa Umwagiliaji wa Ruaha Mbuyuni unaotekelezwa kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFRP-P4R).
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa zoezi la kuurejesha mto Lukosi kwenye mkondo wake wa asili na kubaini kuwa utekelezaji huo umesaidia kurejea kwa shughuli za kilimo cha Umwagiliaji,zilizokuwa zimesimama kwa takribani miaka mitatu.
Akizungumza na wakulima wa Chama cha Umwagiliaji Ruaha Mbuyuni, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Salome Mallamia, alisisitiza umuhimu wa wakulima kutumia ipasavyo miundombinu iliyoboreshwa na kuzingatia usimamizi wa skimu hiyo ili kuongeza uzalishaji na kipato.

“Ada ya huduma ya Umwagiliaji ni shilingi 50,000 kwa ekari kwa msimu mmoja. Kupitia uwepo wa bwawa, mashamba na matumizi ya kilimo cha kisasa, mkulima anaweza kuongeza uzalishaji kutoka magunia 17 hadi kufikia magunia 55 au zaidi kwa ekari moja. Lakini unachotakiwa ni kusikiliza na kufuata maelekezo ya bwana shamba... msipande kama alivyokufundisha shangazi, bibi na babu, Lima katakana....” alisema Mallamia.
Kupitia urejeshaji wa mto na maboresho ya miundombinu ya Umwagiliaji , wakulima sasa wana uhakika wa upatikanaji wa maji, hali iliyopunguza changamoto za awali na kuongeza ushiriki wa wakulima wengi zaidi, hususan wanawake, katika shughuli za kilimo.
Wakulima wa Ruaha Mbuyuni wametoa shukrani kwa Serikali kupitiaTume ya Taifa ya Umwagiliaji na Benki ya Dunia kupitia mradi wa TFRP-P4R kwa kufanikisha urejeshaji wa mto na kuboresha miundombinu ya Umwagiliaji, hatua ambayo imewezesha kurejea kwa kilimo, kuimarika kwa uzalishaji na kuongeza ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo.
Kwa niaba ya wakulima hao, Sulemani Mada alisema kurejea kwa mto kumerejesha uzalishaji na kuwawezesha wakulima wengi kurejea mashambani, huku akibainisha kuwa sasa wanawake wamejikita zaidi katika shughuli za kilimo kutokana na uhakika wa maji na mfumo bora wa usimamizi wa skimu.

Aidha, mkulima Zamda Salum alieleza kuwa hapo awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kugawana zamu za umwagiliaji, hasa nyakati za usiku, lakini baada ya maboresho yaliyofanywa kupitia mradi huo, utaratibu umeimarika na sasa wanapata maji kwa wakati unaofaa, hali inayowezesha wakulima wengi zaidi, wakiwemo wanawake, kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.
Kwa upande wake mzalishaji wa miche ya mazao mbalimbali ikiwemo nyanya, hoho na mboga mboga, Bw. Juma Athuman, amesema kurejea kwa mto kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji wa miche, akibainisha kuwa hapo awali alitumia hadi shilingi 150,000 kwa mwezi kwa ajili ya maji katika uzalishaji huo, lakini sasa gharama hizo zimepungua hadi kufikia shilingi 2,800 kwa mwezi.
“Tumerudi maisha yetu ya kawaida ya awali kabla ya mto kuhama mkondo wake wa asili, kwa sasa uzalishaji unaendelea kwa uhakika zaidi tunashukuru sana,”amesema.

