Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

NIRC, PPRA WASHIRIKIANA KUSIMAMIA SHERIA ZA MIKATABA ILI KUONGEZA TIJA KATIKA MIRADI YA UMWAGILIAJI


 

📍 NIRC – Iringa

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wameona haja ya kuongeza nguvu ili kusimamia sheria za mikataba katika miradi ya Umwagiliaji.

Hatua hiyo imebainika mkoani Iringa katika muendelezo wa mafunzo ya usimaizi wa sheria za mikataba katika miradi ya Umwagiliaji.

Akizungumza katika mafunzo hayo, yanayojumuisha Usimamizi wa Mikataba, Sheria za Ununuzi na Utafiti wa Miamba, Bw. Yahya Amour, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi NIRC, amesema mafunzo hayo yamegusa maeneo nyeti kuanzia usanifu, ununuzi, majadiliano ya mikataba, hadi usimamizi wake.

“Mafunzo haya yatabadilisha mtazamo wa wasimamizi wa miradi. Yatatujengea uwezo wa kufanya uchambuzi sahihi, kusimamia wakandarasi kwa weledi, na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana. Changamoto za awali katika udhibiti wa wakandarasi sasa zinapata suluhisho kupitia elimu hii kutoka PPRA,” amesema Bw. Amour.

Ameongeza kuwa uelewa wa kisheria ni lazima uende sambamba na utaalamu wa kiufundi, hasa ikizingatiwa kuwa NIRC kwa sasa inasimamia ujenzi wa mabwawa makubwa na miundombinu ya Umwagiliaji kote nchini. Mabwawa haya, yanayotarajiwa kukamilika kati ya Machi na Mei mwaka huu, yanahitaji usimamizi makini ili kuzuia upotevu wa fedha na kuhakikisha usanifu wa miamba unatekelezwa kwa usahihi.

Amesema hatua hiyo imezingatia mkakati wa NIRC wa kujenga mabwawa yenye uimara wa kudumu kwa zaidi ya nusu karne, sambamba na azma ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kulifanya kilimo cha Umwagiliaji kuwa chenye tija na uhakika kwa Watanzania.

Naye Mhandisi Yahya Idrisa Manager wa Compliance PPRA amesema taasisi hiyo ilipokea ombi la NIRC kutaka kukaguliwa hatua ambayo haifanywi na taasisi nyingi za Umma kwa kuhitaji kukaguliwa ili kujitathimini.

“Kutokana na hatua hiyo tumeendelea kufanya kazi kwa karibu na NIRC ndio maana leo tuko hapa tumekutana ili kuendelea kushirikiana kuhakikisha
tunasimamia sheria za mikataba katika miradi ya Umwagiliaji,”amesema.


Amesema lengo ni kuhakikisha taratibu za kisheria zinazingatiwa kikamilifu ili kulinda thamani ya fedha na kuimarisha uimara wa miundombinu ya Umwagiliaji. 


Kwa upande wake Mhandisi Lucia Chaula, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Ruvuma, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kubaini maboresho muhimu katika hatua za tathmini ya wakandarasi.

“Uwezo wa kuandaa michoro na usanifu bora utapunguza changamoto wakati wa utekelezaji na kuhakikisha ubora wa kazi unalindwa kisheria kupitia mikataba,” amesema.

Aidha  Mhandisi Nicholaus Ngomai, Msimamizi wa Mradi wa Skimu ya Ilemba mkoani Sumbawanga, amebainisha kuwa awali kutofahamu vyema sheria za ununuzi kulikuwa changamoto kwa wahandisi wengi wa mikoani.

“Semina hii imetupa weledi wa kufuata taratibu zote za kisheria zinazotakiwa na PPRA kuanza kuanzia mwanzo wa mradi. Elimu ya utafiti wa miamba sasa imeunganishwa na usimamizi wa mikataba ili kuhakikisha miradi haina mianya ya kisheria au kiufundi,” amesema.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwajengea wataalamu wa NIRC uwezo wa ndani wa kufuatilia kwa karibu miradi ya Umwagiliaji na kuhakikisha kila senti iliyowekezwa na Serikali inaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Hatua hiyo inafikiwa huku Mkurugenzi Mkuu wa NIRC Raymond Mndolwa akisisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuwa na weledi kwa watumishi katika nyanja za mikataba, ununuzi na miamba ndio utakaofanya miundombinu ya Umwagiliaji kuwa mkombozi wa kweli kwa wakulima wa Kitanzania,” amesisitiza Mhandisi Ngomai.

Kwa kuimarisha uelewa wa sheria na usimamizi wa mikataba, NIRC inajipambanua kama taasisi yenye weledi na uwajibikaji, inayolinda rasilimali za umma na kuhakikisha miradi ya Umwagiliaji inakuwa chachu ya mageuzi ya kilimo nchini.