Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

NIRC NA BENKI YA DUNIA WAFANYA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI YA TFSRP-P4R) TABORA


📍 Tabora

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imefanya mapitio ya utekelezaji wa mradi wa Mifumo  Himilivu ya Chakula (TFSRP-P4R) katika Usimaizi, Uendeshaji na Matunzo katika miradi ya Umwagiliaji katika Mkoa wa Tabora, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba iliyosainiwa kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Vyama vya Umwagiliaji.

Zoezi hilo lilihusisha ziara ya kutembelea katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mwamapuli wilayani Igunga na Skimu ya Umwagiliaji ya Idudumo wilayani Nzega, ambapo maafisa wa NIRC na Benki ya Dunia waliambatana na viongozi wa vyama vya Umwagiliaji pamoja na wakulima wanufaika wa miradi hiyo.

Lengo la mapitio hayo ni kutathmini utekelezaji wa majukumu ya kila upande kwa mujibu wa mikataba 23 iliyosainiwa, mikataba ambayo imeainisha majukumu na wajibu wa NIRC pamoja na vyama vya Umwagiliaji katika mradi wa Mifumo  Himilivu ya Chakula (TFSRP-PforR) katika Usimaizi, Uendeshaji na Matunzo katika miradi ya umwagiliaji.

Kupitia ziara hiyo, timu za wataalamu wa panda hizo mbili  imeangalia kwa karibu maendeleo ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika skimu husika, ikiwemo hali ya miundombinu ya Umwagiliaji pamoja na namna mikataba hiyo inavyotekelezwa katika ngazi ya NIRC, wakulima na vyama vya Umwagiliaji.

Aidha, changamoto zilizobainika wakati wa ziara hiyo zitajadiliwa kwa kina katika vikao vya wataalmu hao, ambapo baada ya majadiliano , pande husika zinatarajiwa kuandaa mpango mkakati wa kutatua changamoto hizo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji.

Katika skimu ya Umwagiliaji ya Idudumo wilayani Nzega, maafisa wa NIRC na Benki ya Dunia walitembelea maeneo mbalimbali ya mradi ikiwemo miundombinu ya Umwagiliaji na bwawa, huku wakipata maelezo ya utekelezaji wa shughuli zinazoendelea kutoka kwa wahandisi wa mradi na wadau wa eneo hilo.

Vilevile, timu ilitembelea skimu ya Umwagiliaji ya Mwamapuli iliyopo katika Kijiji cha Mwanzugi, Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora, ambapo Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kuboresha na kuendeleza skimu hiyo ili kuongeza eneo linalomwagiliwa na idadi ya wakulima wanufaika.

Mapitio hayo yanafanyika kupitia Mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R) unaolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua kipato cha wakulima.