Habari
NIRC NA WADAU WAJADILI UTEKELEZAJI MRADI WA TIRP2 UNAODHIBITI MAFURIKO KUNUSURU MIUNDOMBINU YA RELI
📍NIRC:Dodoma.
Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wadau wanaoshiriki mradi wa kudhibiti mafuriko ili kulinda miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) na ya zamani (MGR), kupitia mradi wa TIRP2 wamekutana kujadili namna ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huo.
Akiongoza kikao kazi hicho Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umwagiliaji Mhandisi Athumani Kilundumya, kutoka katika Wizara hiyo amesisitiza haja ya wadau hao kujadili namna bora ya utekelezaji wa mradi.
_1771922063.jpeg)
Aidha wadau wengine ni viongozi na wataalmu kutoka Wizara Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, akiwemo Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa,wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha, Shirika la Reli, viongozi ofisi ya Mkoa wa Morogoro na Dodoma kwa kushirkiana na Mshauri elekezi ambaye amefanya Upembuzi Yakinifu kuhusu utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa TIRP2 unahusisha ujenzi wa mabwawa sita, pamoja na kuangalia mabwawa mbadala ambayo yatazuia na kupunguza athari za mafuriko kwenye miundo mbinu ya Reli hatua ambayo pia ilikuwa ikisababisha maafa kwa wananchi:
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Katibu, Mhandisi Kilundumya, amesema kuwa awali mradi huo ulipanga kuwapo kwa ujenzi wa mabwawa sita na kuona namna ya kuwapo kwa mabwawa mengine mbadala.
“Tunashukuru Mshauri Elekezi wa mradi kwa kuona haja ya kuwapo mabwawa hayo Sita na kufanya tafiti za upembuzi yakinifu ambazo zimeonyesha kuwa mabwawa 10 yanahitajika ambayo ni mabwawa mbadala.
“ Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa kutoka katika ukarabati mdogo hadi kuwa na suluhisho kubwa na la kudumu, linaloweza kustahimili mafuriko kwa zaidi ya miaka 1,500,”amesema.
Naye, Mkurugenzi Mkuu NIRC, Raymond Mndolwa amebainisha umuhimu wa kuzingatia kipaumbele cha mabwawa hayo kulingana na mchango wa NIRC katika kupunguza mafuriko.

Amesema, katika utekelezaji wa mradi huo, mabwawa yenye athari kubwa zaidi yatapewa nafasi ya kwanza ili kuhakikisha rasilimali na bajeti zinatumika kwa ufanisi.
“Mabwawa yaliyopo kutokana na kukaa kwa muda mrefu yamepunguza mchango wake katika kudhibiti mafuriko, hivyo utekelezaji wa mradi huu utasaidia kulinda Reli yetu, sekta ya Kilimo kwa kuwa na akiba ya maji ya kutosha kwa ajili ya Umwagiliaji na kuokoa maisha ya wananchi na kuleta ufanisi wa kiuchumi na kiusalama”, amesema
Wataalamu walioshiriki kikao hicho pia wamebainisha kuwa mkakati wa kiufundi unaonyesha kuwa tatizo kubwa la mafuriko linatokana na maeneo ya juu ya mito yanayobeba maji mengi, tope na magogo makubwa yanayotishia madaraja na kwamba mabwawa mapya ya juu ya mto yapewe kipaumbele ili kupunguza athari hizo.
Wameongeza kuwa, njia mbadala kama dredging, miradi ya Umwagiliaji na uelekezaji maji zinaweza kutumika kudhibiti madhara ya mafuriko kwa jamii na kulinda miundombinu ya reli.
Wadau hao pia wamejadili masuala ya kijamii na mazingira na kushauri kuwapo kwa umuhimu wa maeneo hayo kupewa uzito mkubwa kabla na wakati wa utekelezaji wa mradi huo.


