Habari
WAKULIMA MANG'OLA WAFIKIWA ELIMU YA USIMAMIZI, UENDESHAJI NA MATUNZO MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI
š NIRC Karatu, Arusha.
Wakulima skimu ya Umwagiliaji Mang'ola Barazani iliyopo wilayani Karatu Mkoani Arusha wameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kuwapatia mafunzo ya Uendeshaji, Usimamizi na Matunzo ya skimu za Umwagili hali itakayochangia miundombinu inayoendelea kujengwa na Serikali kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Wakulima hao wametoa kauli hiyo wakati wa mafunzo hayo yanayotolewa na wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji yanayolenga kujenga uelewa kwa wakaulima kutambua wajibu wao katika usimamizi na utunzaji miundombinu ya Umwagiliaji.
Wilfred Gidion ni miongoni mwa wakulima waliopatiwa mafunzo hayo ambapo amesema, yatwasaidia kulinda miundombinu ya Umwagiliaji na kudhibiti upotevu wa maji unaotokana na uharibifu wa miundombinu hiyo.

Aidha amesema hali hiyo itachangia maji kupatikana kwa wakati hali itakayoongeza upatikanaji wa mavuno.
“Hatua ya ukarabati wa skimu unaoenda kufanywa pia utaongeza eneo la Umwagiliaji na kuleta tija kwa wakulima na kuinua vipato vya wakulima na kuwa na uhakika wa chakula.
Kwa upande wake Sabina Njiro, amesema awali hawakuwa na ufahamu wa majukumu yao katika utunzaji na usimamizi wa miundombinu ya Umwagiliaji na waliamini walikuwa na jukumu hilo ni Serikalkali kupitia Tume hivyo kwa sasa watahakikisha wanatunza miundombinu hiyo.
Amesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa katika mgawanyo wa majukumu na kuitunza miundombinu ya Umwagiliaji, kwani elimu hiyo imetoa mwongozo wa matunzo, usimamzi na uendeshaji wa Skimu hivyo itasaidia kuongeza tija katika Kilimo.
Kwa upande wao wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akiwemo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendeshaji Salome Njau, ameleeza kuwa, mafunzo hayo kwa wakulima ni muendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP - P4R).

Amesisitiza mradi huo, unalenga kuwasaidia wakulima kuwa na kilimo cha uhakika kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Aidha utekelezaji wa mradi huo utahakikisha azma ya Serikali ya Agenda10/30 inafikiwa.
“Lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na ghala la chakula kutokana na uzalishaji wa mazao kupitia kilimo cha uhakika,”amesema.
Sanjari na hayo wakulima pia wamepatiwa elimu ya Sheria ya Umwagiliaji juu ya umuhimu wa uchangiaji ada ya huduma za Umwagiliaji.
Afisa Sheria wa Tume. Amina Mweta, amesema katika mgawanyo wa majukumu kati ya Tume na wakulima, wakulima wamepatiwa elimu ya utiaji saini mkataba wa Uendeshaji, Usimamizi na Matunzo ya skimu za umwagiliaji.


