Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

WANANCHI MBULU MJINI   WASISITIZWA KUTUNZA NA KUITHAMINI MIUNDOMBINU YA MRADI WA VISIMA VYA UMWAGILIAJI


 

📍 Mbulu - Manyara.

Wananchi wa halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara wasisitizwa kutunza miundombinu ya mradi wa uchimbaji visima vya Umwagiliaji ili kuhakikisha mradi huo unaleta tija katika kukuza sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji nchini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael John Semindu   wakati wa hafla ya uzinduzi mradi wa uchimbaji visima iliyofanyika katika kijiji cha Tiwiti kata ya Gehandu.

Amesema lengo la Serikali ni kukuza pato la mkulima mmoja mmoja  kwa kuongeza kipato na kuwasaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mhe. Semindu  amewaeleza Wananchi  kuwa lengo la Serikali ni kukuza pato la mkulima mmoja mmoja,kuongeza kipato na kuwasaidia wananchi kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa mvua chache msimu wa kilimo.

“Kwa Pamoja tunao wajibu wa kulinda na kutunza miundombinu yote ya mradi,hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwingine ili iweze kudumu na kizazi kijacho hii pia ni moja ya kuunga mkono juhudi za serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali itaonekana, alisisitiza Mhe. Semindu

Kwa upande wake Afisa Kilimo Kutoka Tume ya Umwagiliaji Wilaya ya Mbulu Bw. Japheth Nyankale  amesema jumla ya visima vitano (05) vitachimbwa katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu huku akiwaomba Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu  kutoa ushirikiano  katika kipindi cha utekelezaji wa mradi  na amewaeleza wananchi ambao watapisha maeneo ya utekelezaji  wa mradi  serikali itafuata utaratibu wote na kuhakikisha wananchi hao  wanalipwa fidia.

Aidha Bw. Nyankale amesema kuwa awamu ya kwanza ya mradi inahusisha uchimbaji wa visima katika vijiji 10 vya wilaya ya Mbulu, kila kisima kikihudumia zaidi ya ekari 40 za mashamba.

Amesema mradi huo unalenga  kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha wakulima wana uhakika wa kilimo cha msimu zaidi ya mmoja.

Naye, Diwani mteule wa Kata ya Gehandu Mhe. Alex Tango ametoa Shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza mradi  kubwa na wenye tija kwa Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, ameeleza kuwa mradi utapunguza gharama za maisha zitokanazo na uhaba wa chakula.

Hata hivyo wananchi wa  kata ya Gehandu wameishukuru Serikali kwa mradi wa Visima vya umwagiliaji  ambapo itasaidia kupunguza au kuondokana na changamoto ya Maji katika shughuli za kilimo na matumizi mengine ya nyumbani.