Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

MNDOLWA AAGIZA USIMAMIZI MADHUBUTI WA SKIMU ZA UMWAGILIAJI


Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amewaagiza Mameneja skimu pamoja na Mafundi Sanifu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufuata misingi ya usimamizi skimu za umwagiliaji na kuhakikisha wanaongeza tija kwa wakulima katika skimu wanazosimamia.

Mndolwa ametoa maagizo hayo wakati akifungua mafunzo ya miradi inayoratibiwa na Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP - P4R) kwa mameneja wa skimu pamoja na mafundi sanifu yanayofanyika mkoani Morogoro yaliyolenga kuwajengea uwezo wataalamu hao juu ya mfumo endelevu wa usimamizi na matunzo ya skimu za umwagiliaji.



Amesema ni wajibu kwa wataalamu hao kuzingatia misingi ya usimamizi wa skimu kwani serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umwagiliaji.

"Mkiangalia historia ya nchi hii kabla ya serikali ya awamu ya sita kumekuwa na jitihada nyingi sana za uwekezaji kwenye sekta ya umwagiliaji kwani haijawahi kutokea kwenye nchi hii uwekezaji wa aina hii kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita, sasa leo hii tunafanya kazi kubwa sana ya kufanya ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, ni jukumu lenu ninyi kuwa sehemu ya uandaaji mashamba ya wakulima na kuwa sehemu ya kuwasimamia wakandarasi wanaofanya zile kazi na kuhakikishamiradi hiyo inaishi kwa muda mrefu". Amesema Mndolwa.



Kwa upande wake Mratibu Mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP - P4R) mhandisi Naomi Mcharo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula ambapo umuhimu wa mafunzo hayo kwa Mameneja skimu za Umwagiliaji na Mafundi Sanifu ni wataalamu hao kuongeza ujuzi wa mfumo endelevu wa usimamizi na matunzo ya skimu za umwagiliaji, ambapo mafunzo hayo yameainisha hatua mbalimbali za kufuata ili kuwa na miradi itakayodumu na kuongeza tija katika kilimo cha umwagiliaji.



Aidha utekelezaji wa mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP - P4R) utaongeza tija na mchango uwekezaji wa serikali unaolenga kupunguza athari zinazotokana na uhaba wa maji kwenye mifumo ya Umwagiliaji iliyopo na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna.