Habari
MIRADI YA UMWAGILIAJI YALETAÂ MAPINDUZI KWA WAKULIMA TABORA NA SINGIDA
📍Tabora, Singida
Miradi ya Umwagiliaji inayotekelezwa na Serikali imeendelea kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wakulima kwa kuongeza mavuno, kipato na kuimarisha usalama wa chakula.
Hatua hiyo imebainika wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa David Silinde, alipotembelea miradi ya ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya Umwagiliaji katika mikoa ya Tabora na Singida, ambapo wakulima walionesha mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali, kupitia miradi ya Umwagiliaji.
Mkoani Tabora, katika skimu ya Umwagiliaji ya Mwamapuli, Mheshimiwa Silinde alishuhudia mafanikio ya wakulima wa mpunga kupitia Chama cha Ushirika cha Umwagiliaji Mwamapuli (AMCOS), chenye wanachama 970.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kupitia uwekezaji katika kilimo cha Umwagiliaji Mkoani Tabora, Serikali imechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa Mpunga, kutoka tani 2.5 hadi tani 7.5 kwa hekari moja, huku wakulima wakifanikiwa kumiliki zana za kisasa za kilimo ikiwemo trekta, rotaveta, mashine tatu za kuvunia mpunga na mashine ya kukoboa, hatua iliyopunguza gharama za uzalishaji katika kilimo na kuongeza ufanisi.

Amesema, miradi hii ya Umwagiliaji imeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wakulima kwa kuongeza mavuno, ajira na kipato sambamba na dhamira ya Serikali ya kuboresha sekta ya kilimo kupitia kilimo cha Umwagiliaji , kwa lengo la kumuinua mkulima mmoja mmoja.
Amesema, Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuelekeza fedha katika uendelezaji wa miundombinu ya Umwagiliaji, hatua inayochochea mapinduzi ya kilimo na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wa wakulima wa Mwamapuli wametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia, kwa kuendelea kuwaunga mkono kupitia ruzuku ya mbolea na upanuzi wa skimu ya Umwagiliaji,uliowanufaisha pia vikundi vya Mahambasi A na B pamoja na Makomero A na B.
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeeleza kuwa mradi wa upanuzi wa skimu hiyo unaongeza eneo la Umwagiliaji kutoka hekta 630 hadi hekta 2,565 na unatarajiwa kuwanufaisha wakulima wapatao 5,000, hatua itakayoongeza uzalishaji na kipato kwa wananchi.
Kwa upande wa Mkoa wa Singida, Naibu Waziri alitembelea Mradi wa Umwagiliaji Msingi unaotekelezwa katika Kijiji cha Ishinsi, Wilaya ya Mkalama.

Mradi huo unagharama ya shilingi bilioni 34.1 unatarajiwa kumwagilia zaidi ya ekari 2,000 na kunufaisha wakulima 5,000 pamoja na wakazi zaidi ya 12,000 wa vijiji nane.
Ujenzi huo unatekelezwa na mkandarasi Nakuroi Investment Company, kwa miezi 18 na utekelezaji wake ni kuanzia Juni 2023 hadi Oktoba mwaka huu.
Aidha mazao yanayotarajiwa kulimwa katika miradi hiyo ni mpunga, mahindi, alizeti na vitunguu, huku uzalishaji wa mpunga ukitarajiwa kufikia gunia 45 hadi 50 kwa ekari moja.
Hadi kufikia Desemba mwaka 2025, utekelezaji wa mradi wa Umwagiliaji Msingi umefikia asilimia 60 ya utekeleza wake, ambapo ujenzi wa ofisi ya mradi umekamilika kwa asilimia 95, miundombinu ya mashambani kwa asilimia 70 na barabara za mashambani kwa asilimia 80.
_1768308319.jpeg)

