Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

NIRC YAUNGANISHA WADAU WA MAZINGIRA KUOTESHA MITI 3,000 KATIKA VYANZO VYA MAJI KILOLO


NIRC YAUNGANISHA WADAU WA MAZINGIRA KUOTESHA MITI 3,000 KATIKA VYANZO VYA MAJI KILOLO

📍NIRC Kilolo Iringa.

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imepanda miti 3,000 katika Kijiji cha Ruaha Mbuyuni, Wilaya ya Kilolo, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kulinda mazingira na rasilimali za maji, katika maeneo yanayo zunguka Skimu za Umwagiliaji nchini.

Tume imefanya hayo kwa kushirikisha wadau mbali mbali ikiwepo  Benki ya Dunia, kupitia Mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula Nchini(TFSRP), Wakala wa hifadhi ya Misitu(TFS), Mamlaka ya Bonde la Mto Ruaha, Halmashauri ya Kilolo na Wananchi wa Kilolo.

Hatua hii inalenga kuhifadhi uoto wa asili, kuimarisha ikolojia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Estomin Kyando, amewataka wananchi wa Ruaha Mbuyuni kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa kwa manufaa ya sasa na ya baadae. 

Ameongeza kuwa jitihada za kulinda mazingira na vyanzo vya maji ni msingi wa kupunguza mmomonyoko wa udongo na kutunza vyanzo vya maji, na kwamba ili kufanikisha hilo, wananchi wanapaswa kupanda miti ambayo ni rafiki na maji

Kwa upande wake, Afisa Mazingira na Jamii kutoka NIRC, Bi. Eveta Kayingi, amesema upandaji miti ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuhakikisha miradi ya  Umwagiliaji inakwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Ameongeza kuwa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza miti itaendelea kutolewa ili kuhakikisha miti hiyo inakua na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wao, Wananchi wa Ruaha Mbuyuni wamepongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa upandaji miti utaboresha mazingira yao, kuongeza kivuli, na kulinda ardhi dhidi ya mmomonyoko. 

Wananchi hao wameahidi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miti iliyopandwa, wakitambua kuwa jukumu la uhifadhi ni la kila mmoja.

Kupitia kampeni hiyo, NIRC imedhihirisha kuwa kulinda vyanzo vya maji si jukumu la serikali pekee bali ni wajibu wa kila mmoja. 

Hatua hiyo inaleta matumaini ya Kilolo kuwa mfano wa wilaya inayojali mazingira na kuwekeza katika mustakabali wa kizazi kijacho.