Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

WAKULIMA MVUMI WAISHUKURU NIRC KUWAPATIA MAFUNZO YA UENDESHAJI, USIMAMIZI NA MATUNZO YA SKIMU


 

📍 NIRC Kilosa, Morogoro.

 

Wakulima skimu ya umwagiliaji Mvumi iliyopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro wameishukuru serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kuwapatia elimu ya uendeshaji, usimamizi na matunzo ya skimu kwani hatua hiyo inaonesha nia ya dhati ya serikali kuhakikisha miundombinu inayoendelea kujengwa inalindwa dhidi ya uharibifu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo  yanayotolewa na wataalamu wa Tume kupitia mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R), Makamu Mwenyekiti wa skimu hiyo Bw. Lazaro Amoni amesema kwa kipindi cha miaka mitatu wamekuwa wakitaabika kutokana na  uharibifu wa miundombinu ya umwagiliaji, kutokana na kukosa weledi katika usimamizi, uendeshaji na utunzaji miundombinu hiyo.

Amesema katika skimu hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kujaa kwa mchanga katika banio, mfereji mkuu kujaa mchanga pamoja na  mifugo kuingia mashambani.

Amesema hali hiyo inasababisha changamoto ya maji kutokufika mashambani na kupoteza rutuba mashambani kutokana na mchanga unaokuwa katika mifereji.

 

 

Amesema sambamba na elimu waliyopatiwa juu ya Uendeshaji, usimamizi na utunzaji wa skimu, skimu hiyo kuwa miongoni mwa skimu 23 zitakazonufaika na mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R), itasaidia kuondokana na changamoto hiyo pamoja na kudhibiti uharibifu wa miundombinu.

Kwa upande wake Bi Lakelo Mkandawile,  mkulima wa skimu hiyo amesema kwa kipindi kirefu skimu hiyo imekuwa ikiendeshwa kienyeji  hivyo mafunzo hayo yatasaidia kutunza miundombinu hiyo na kutambua wajibu wao katika kuhakikisha miundombinu hiyo inaleta tija katika kilimo na kuinua uchumi wao.

Aidha ameishukuru serikali kwa kuichagua skimu hiyo kunufaika na mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R), kwani itasaidia kukarabati sehemu zilizoharibika na kufikia malengo ya serikali kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula.

Aidha, katika mafunzo hayo wakulima wamekumbushwa kutunga sheria ndogo zinazolinda miundombinu ya umwagiliaji dhidi ya uharibifu, ikiwemo kudhibiti mifugo kuingia mashambani na kudhibiti wakulima kulima kando ya miundombinu ya umwagiliaji.

 

 

Sanjari na hayo wakulima hao pia wamepatiwa elimu ya Mfumo wa Kielektroniki wa  Usimamizi Shughuli za Umwagiliaji (iMIS) unaolenga katika kukusanya takwimu za uzalishaji, kuhifadhi taarifa za ukubwa wa mashamba na kukusanya taarifa za idadi ya wakulima kwa umri na jinsia.

Aidha wakulima pia wamepatiwa elimu ya umuhimu wa utiaji saini mkataba wa Uendeshaji, usimamizi na matunzo unaoainisha mgawanyo wa majukumu kati ya Tume na wakulima katika ukarabati miundombinu ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula.