Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

BODI NIRC MGUU SAWA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE


 

Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imesema inatambua dhamana iliyonayo katika kutekeleza majukumu yake na mkakati wa ubunifu katika kufanikisha dira na dhima ya Tume.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Richard Masika, katika mafunzo ya muundo wa Bodi, kanuni na taratibu za uendeshaji pamoja na majukumu ya yake.

 



Amesema mafunzo hayo ni muhimu ili viongozi kwa pamoja waelewe wajibu walionao na nafasi ya Bodi katika taasisi.

Dkt. Masika ameongeza kuwa, kwa mujibu wa muktadha wa utaratibu bora, Bodi hiyo inatumia sheria, sera, kanuni, taratibu na utaalamu wa menejimenti, kuongoza katika kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya umma.



Dkt. Masika amesema, Bodi ina wajibu katika kusimamia Tume, Menejimenti na Rasilimali, ili kuhakikisha malengo yanafikiwa, hivyo, mafunzo hayo yatasaidia kufikia azma hiyo.

Pia, amehimiza ushirikiano kati ya Bodi na Menejimenti kwa kuwa ni timu moja na wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kufikia malengo yaliyopo na kukuza sekta ya kilimo cha Umwagiliaji nchini.


Dkt. Masika amemshukuru Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yana tija katika kusimamia mustakabali wa sekta ya kilimo nchini.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Maria Itembe, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa pande zote mbili,Bodi ya Uongozi na Menejimenti, kwa kuwa yataongeza chachu katika utendaji wa kila siku wa Tume.