Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

WATAALAMU NIRC WAASWA KUZINGATIA SHERIA MPYA YA MANUNUZI KATIKA USIMAMIZI WA MIRADI



šŸ“ Dodoma

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amewataka wahandisi umwagiliaji wa mikoa, ambao ni wasimamizi wa miradi ya umwagiliaji katika mikoa husika, kufuata sheria na kanuni za sheria ya manunuzi katika usimamizi wa miradi ya umwagiliaji.

Mndolwa ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya Sheria Mpya ya Ununuzi Namba 10 ya Mwaka 2023 na Kanuni za mwaka 2024,kwa Wajumbe wa Bodi ya Zabuni, wahandisi wa umwagiliaji wa mikoa na Afisa Masuuli; ambapo amewakumbusha kuwa jukumu lao si tu kusimamia miradi bali kusimamia miradi kwa kuzingatia matakwa ya sheria za manunuzi.

“Ndani ya kazi ya umma hakuna nia njema kuna utaratibu, niwaombe sana tufuate taratibu tusimamie kazi zetu, hii sheria ambayo mnakumbushwa mjione ninyi ni watendaji wakuu katika mikoa yenu." Amesema Mndolwa.

 



Aidha Mndolwa amewasisitiza wahandisi wa umwagiliaji kuhakikisha wanasimamia miradi itakayodumu kwa muda mrefu ili iwe na tija katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji nchini.

“Mradi mzuri wa umwagiliaji lazima uishi sio chini ya miaka 20 bila ukarabati, mjiulize maswali mnaosimamia miradi je mradi ninaosimamia utadumu zaidi ya miaka 20 bila ukarabati" alisisitiza Mndolwa.

Hata hivyo Mndolwa ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji hivyo ni wajibu kusimamia miradi ya Umwagiliaji ili kuleta tija katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji.

Baadhi ya wahandisi Umwagiliaji walioshiriki mafunzo hayo wameeleza matarajio yao kutokana na mafunzo watakayopatiwa na kukiri kuwa yatawasaidia katika usimamizi wa miradi itakayoleta tija na kufikia azma ya serikali.

Mafunzo hayo ya Sheria Mpya ya Manunuzi yametolewa na wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununzi wa Umma (PPRA), na yamelenga kujenga uwezo wa ununuzi na usimamizi wa mikataba, kuongeza ufahamu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kanuni za mwaka 2024, pamoja na kuhakikisha Tume inafikia malengo tarajiwa katika miradi yake ya kimkakati.